
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani limefanya ukaguzi wa mabasi 40 yanayofanya safari za mikoani na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mabasi matano (5) yaliyobainika kuwa na hitilafu za kiufundi zinazoweza kuhatarisha maisha ya abiria.
Akizungumza wakati wa operesheni hiyo endelevu ya ukaguzi na utoaji elimu ya usalama barabarani, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Yusufu Kamota amesema mabasi hayo 5 yamesitishiwa safari na kufungiwa hadi yatakapokamilisha matengenezo muhimu kwa mujibu wa sheria.
SSP Kamota ametoa wito kwa wamiliki na madereva wa vyombo vya usafiri kuhakikisha magari yao yanakaguliwa na kuwa katika hali salama kabla ya kuingia barabarani, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kudhibiti ajali zinazoweza kuleta madhara makubwa ikiwemo vifo, ulemavu wa kudumu na majeraha kwa wananchi.
Aidha, Kamota ametoa onyo kali kwa madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani, wakiwemo wanaotumia vilevi wakiwa kazini na wale wanaojihusisha na "beting" — aina ya ushindani wa mwendo mkali barabarani bila kujali usalama wa abiria.
"Msifanye mashindano mnapoendesha vyombo vya usafiri. Kumbukeni abiria mnaowabeba wanategemewa na familia zao na taifa kwa ujumla. Kufanya hivyo ni kinyume na sheria na tutachukua hatua kali bila muhali," amesema Kamota.
Kwa upande wao, baadhi ya abiria wamepongeza Jeshi la Polisi kwa hatua hiyo wakisema inaleta matumaini ya usalama wa safari zao. Wametumia nafasi hiyo kuonya baadhi ya wamiliki wa mabasi wanaowapa madereva magari mabovu kwa lengo la kujinufaisha kifedha bila kujali usalama wa abiria.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano – Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma

















No comments:
Post a Comment