OR - TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais TAMISEMI Prof. Tumaini Nagu amewataka Maafisa Lishe kuimarisha elimu ya lishe kwa jamii ili kudhibiti udumavu na ukondefu kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 pamoja na uzito uliopitiliza kwa watu wazima.
Prof. Nagu ametoa agizo hilo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa uratibu wa masuala ya lishe nchini kwa maafisa lishe wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa waliokutana Jijini Dodoma kwa muda wa siku mbili kujadili namna ya kufanya maboresho katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.
Katika maelekezo yake kwa watendaji hao, Prof. Nagu amesema Taifa linawategemea sana kubadilisha afya za watanzania hasa kwa kutoa elimu zaidi na kuishauri jamii juu ya ulaji bora ili kukabiliana na matatizo ya lishe.
“Nyie ndio jiwe la msingi kuhakikisha kuwa takwimu mbovu za lishe tulizonazo zinabadilika, tufanye kazi kweli ili tuwe na sababu ya kutembea kifua mbele kwamba tumeibadilisha jamii, kwa kuhakikisha tunatoa elimu juu ya ulaji bora na tunatekeleza program zinazowekwa kitaifa zenye lengo la kuboresha afya ya jamii yetu kupitia lishe bora” alisema Prof. Nagu.
Awali akisoma risala ya maafisa lishe hao January Dalushi amewasilisha ombi kwa Serikali na kuielekeza Taasisi ya MSD kuagiza Chakula Dawa ili vituo viweze kununua kwa urahisi, huku wakiomba Maafisa Lishe wawe moja ya Wataalam wanaoajiriwa kwenye Taasisi hiyo ili kutoa ushauri wa kitaalam kwenye bidhaa mbalimbali za Lishe zinazonunuliwa na Bohari ya Dawa ya Taifa.
Ajenda ya lishe inatajwa kuwa miongoni mwa vipaumbele muhimu vya kiuchumi ulimwenguni kote kutokana na athari za matatizo ya lishe katika ukuzaji wa uchumi na kuleta maendeleo endelevu ya ulimwengu ifikapo 2030.
No comments:
Post a Comment