
Kongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, amepongeza uongozi wa Halmashauri ya Arusha kwa kutenga rasmi eneo maalum la michezo katika Kijiji cha Mlangarini, akisisitiza kuwa eneo hilo lisibadilishwe matumizi kwa kuwa limepewa matumaini na wananchi kama kituo cha kukuza vipaji na kuimarisha afya za vijana.
Ussi amesema kuwa hatua hiyo inaunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuinua sekta ya michezo nchini sambamba na kupambana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, huku akiongeza kuwa michezo ni njia salama ya kuwaondoa vijana katika vishawishi vya uhalifu na dawa za kulevya.
“Mradi huu una tija kubwa kwa jamii. Mbali na kusaidia vijana kujihusisha na shughuli chanya, unasaidia pia kupunguza mzigo wa kiafya kwa jamii yetu,” alisema Ussi.
Wananchi wa Mlangarini wameishukuru Serikali kwa hatua hiyo, wakisema kuwa kwa miaka mingi walikuwa na changamoto ya ukosefu wa maeneo ya michezo, jambo lililowakatisha tamaa vijana wengi wenye vipaji.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Elibariki Lema, alisema kuwa eneo hilo limekuja kwa wakati sahihi na linaenda kuleta mapinduzi si tu katika sekta ya michezo, bali pia kiuchumi, kwani michezo sasa ni ajira na chanzo cha mapato.
“Kwa sasa michezo si burudani pekee, bali ni biashara. Tunahitaji kuwaandaa vijana wetu mapema kwa mazingira hayo,” alisema Elibariki.
Kwa mujibu wa Afisa Michezo wa Halmashauri ya Arusha, Mwl. Priscus Silayo, kiwanja hicho kina ukubwa wa mita za mraba 8,642, kimepimwa rasmi kwa namba 548 na kitakuwa na matumizi mbalimbali ikiwemo mashindano ya shule za msingi na sekondari, mazoezi ya kijamii na matukio ya kimichezo.
Aidha, Silayo alibainisha kuwa uwepo wa kiwanja hicho pia utachangia kuongeza mapato ya halmashauri kupitia matukio mbalimbali ya michezo, sambamba na kutumika kama sehemu ya kuibua na kulea vipaji vya ndani.
Mwenge wa Uhuru mwaka huu umebeba ujumbe wa “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu,” huku pia ukisisitiza ushiriki wa vijana katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia sekta ya michezo.





No comments:
Post a Comment