SERIKALI YALIPONGEZA JKT KWA MATUMIZI MAZURI YA FORCE ACCOUNT - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, July 6, 2025

SERIKALI YALIPONGEZA JKT KWA MATUMIZI MAZURI YA FORCE ACCOUNT


Na Benny Mwaipaja, Katavi


Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amelimwagia sifa na kulipongeza Jeshi la Kujenga Taifa kwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi mkubwa kupitia mfumo wa Force Account katika Kiteule cha Tanganyika kinachojengwa kupitia Kikosi cha Jeshi hilo cha Milundikwa kilichoko wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi.

Pongezi hizo zimetolewa kwa niaba yake na Kamishna wa Bajeti kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Meshack Anyingisye baada ya kutembelea na kujionea utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika Kiteule cha Tanganyika, ambayo ni Kambi tarajiwa ya Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa.

Bw. Anyingisye amesema kuwa uzalendo na nidhamu ya matumizi ya fedha uliooneshwa na Jeshi la Kujenga Taifa katika ujenzi wa majengo mbalimbali katika kiteule hicho ambao hadi kukamilika kwake, mradi unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 8.6, unafaa kuigwa na taasisi nyingine za Serikali zinazotekeleza miradi yake kwa njia ya Force Account.

“Miundombinu iliyojengwa hapa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.5 za awali tulizowapatia, na kwa ubora wa hali ya juu, ingekuwa maeneo mengine tungeambiwa fedha hizo zimeisha bila uwepo wa thamani ya fedha husika, kwa niaba ya Ungozi wa Wizara ya Fedha, ninawapongeza sana” Alisema Bw. Anyingisye.

Alisisitiza kuwa utaratibu unaotumiwa na Jeshi la Kujenga Taifa katika ujenzi wa miundombinu yake kwa utaratibu wa matumizi ya fedha bila kutumia zabuni (Force Account), unafaa kuigwa na Taasisi nyingine za Serikali ili malengo ya Serikali ya kuharakisha upatikanaji wa huduma kwa gharama nafuu na kwa ubora wa hali ya juu yaweze kufikiwa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajab Nduku Mabele, Kaimu Mkuu Tawi la Utawala Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa, Kanali Juma Issa Mrai, aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kulipatia fedha Jeshi hilo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yake ya maendeleo.

Alisema kuwa ujenzi wa miundombinu ya Kiteule cha Tanganyika utakapokamilika, utaliwezesha Jeshi la Kujenga Taifa kufungua Kikosi Kipya cha Jeshi hilo kitakacho wezesha kuchukua zaidi ya wahitimu 3,600 wa kidato cha sita kwa wakati mmoja kwa ajili ya mafunzo na uzalishaji.

Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Kiteule cha JKT-Tanganyika, Mkuu wa Kikosi cha 847 KJ-Milundikwa, Kanali Philemon Mahenge, alisema kuwa Kiteule cha Tanganyika kimepokea kutoka Serikalini kiasi cha shilingi bilioni 2.5 zilizotumika kujenga miundombinu, yakiwemo majengo 9 yanayohusisha utawala, mabwalo, mahanga, zahanati na miundombinu mingine ya Jeshi.

Ziara hiyo ya kutembelea mradi wa Kiteule cha Tanganyika uliwahusisha pia Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, Kamishna wa Sera na Mipango, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Bw. Obed Sayore, Kaimu Mkurugenzi wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Kanali E;phraim Kituhile, Mkurugenzi wa Fedha wa JKT, Luteni Kanali Everine Kibisa na Afisa bajeti Wizara ya Ulinzi, Meja Magreti Kakuru.

No comments:

Post a Comment