Mafunzo ya siku tano kwa Maafisa Elimu kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara yameanza rasmi jijini Arusha, yakilenga kuwajengea uwezo viongozi hao katika utekelezaji wa majukumu yao ya kiutendaji.
Mafunzo hayo yalifunguliwa Machi 8, 2026 na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Atupele Mwambene.
Mafunzo hayo yanasimamiwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) kwa kushirikiana na taasisi ya Shule Bora, yakihusisha wataalamu kutoka ADEM pamoja na vyuo vikuu mbalimbali Tanzania Bara.
Miongoni mwa mada zinazotolewa ni pamoja na uongozi bunifu wa kimkakati katika kutatua migogoro, mbinu za kutafuta rasilimali fedha na matumizi sahihi ya rasilimali nyingine, pamoja na umuhimu wa ushirikishwaji katika kuongoza sekta ya elimu. Mada nyingine zinahusu ujifunzaji na uatamizi katika uongozi wa elimu.
Aidha, washiriki wanapatiwa maarifa kuhusu matumizi sahihi ya akili hisia (Emotional Intelligence) ili waweze kutambua, kuelewa na kusimamia hisia zao pamoja na za wengine, hatua itakayosaidia kupunguza msongo wa mawazo, kuboresha mawasiliano, kuimarisha ushirikiano na kuongeza tija katika usimamizi wa sekta ya elimu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mwambene aliipongeza ADEM na Shule Bora kwa kufanikisha maandalizi ya mafunzo hayo na kuwataka washiriki kuyatumia vyema maarifa watakayopata.
Aliwasisitiza viongozi hao kushughulikia kwa umakini malalamiko yanayojitokeza katika maeneo yao ya kazi pamoja na kutekeleza kwa ufanisi malengo ya kisera na mabadiliko ya mitaala.
“Ninawaomba mhakikishe mnaandaa mazingira rafiki ya kujifunza na kujifunzia, na mnasimamia changamoto zinazotokana na malalamiko katika maeneo mnayoyasimamia,” alisema Mwambene.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dk. Maulid J. Maulid, alisema ushirikiano kati ya taasisi hiyo na Shule Bora umefanikisha uandaaji wa matini mbalimbali za mafunzo kwa viongozi wa elimu.
Alizitaja baadhi ya matini hizo kuwa ni pamoja na za uanzishwaji na usimamizi wa Jumuiya za Kujifunzia, usimamizi wa uongozi wa kujifunza, pamoja na mafunzo kwa viongozi wa elimu katika ngazi za mikoa na wilaya.
Dk. Maulid alisema mafunzo hayo yatawasaidia viongozi wa elimu kuwa na maono ya mageuzi makubwa yanayoendana na mabadiliko ya kiteknolojia pamoja na dira ya maendeleo ya Taifa 2050.
Aliongeza kuwa kupitia mafunzo hayo viongozi hao watafahamu umuhimu wa mipango ya kisekta pamoja na namna sahihi ya kutathmini mafanikio na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao.











No comments:
Post a Comment