Diwani wa Kata ya Majengo, Zacharia Soko, amekabidhi mashine ya kisasa ya photocopy yenye thamani ya Sh milioni 3.5 kwa Shule ya Msingi Anderson Msumba, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na kuongeza kiwango cha ufaulu shuleni.
Mbali na mashine hiyo, Diwani Soko amekabidhi vifaa mbalimbali vya shule, ikiwemo karatasi nyeupe (rimu) tano, daftari za mahudhurio (attendance registers) za wanafunzi, boksi tatu za kalamu za bluu, boksi tatu za kalamu nyekundu pamoja na maboksi ya chaki.
Amesema mashine hiyo imekamilika ikiwa na vifaa vyake muhimu na inalenga kupunguza gharama ambazo shule imekuwa ikitumia katika uchapishaji wa mitihani na nyaraka nyingine za kielimu.
Diwani Soko amesema yuko tayari kuendelea kusaidia walimu wanaojitolea katika shule hiyo, akisisitiza kuwa wazazi hawapaswi kubebeshwa mzigo wa michango mbalimbali ambapo amechangia shilingi laki sita kwa ajili ya waalimu watatu na zoezi hili ni endelevu.
“Mimi mwenyewe nitajitahidi kuhakikisha walimu wanaojitolea wanaendelea kuwepo ili watoto waweze kupata elimu, Sitaki wazazi wasumbuliwe kwa michango,” amesema Soko.
Amesema lengo lake ni kuhakikisha Kata ya Majengo inafanya vizuri katika elimu, akibainisha kuwa mafanikio hayo yanawezekana kupitia ushirikiano kati ya viongozi, walimu na wazazi.
Diwani Soko amewataka wanafunzi kuzingatia nidhamu, akisema elimu bila nidhamu haiwezi kuwa na matokeo yanayotarajiwa.
“Elimu bila nidhamu ni bure. Mtoto ambaye hana nidhamu hawezi kufanikiwa katika maisha, hata katika masomo, nidhamu ni pamoja na kufika darasani mapema, kuandika masomo yote na kuhudhuria vipindi vyote,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Msingi Anderson Msumba Scholastika Leonard ameeleza kuwa ujio wa mashine hiyo utasaidia kupunguza gharama za uchapishaji wa mitihani na kuhakikisha wanafunzi wanapata mitihani kwa wakati.
Mkuu wa shule hiyo amesema hapo awali wanafunzi walikuwa wakihitajika kuchangia fedha kwa ajili ya mitihani, lakini kutokana na msaada huo, kuanzia mitihani ya mwaka huu hali hiyo itabadilika.
“Kwa kupitia msaada wa Mheshimiwa Diwani, mitihani ya mwezi wa tisa na mwezi wa kumi na mbili mwaka huu itafanyika bila wanafunzi kuchangia fedha, Hatutaki mtoto aende nyumbani kuomba fedha za mtihani,” amesema Scholastika.
Mwanafunzi wa shule hiyo, Masele Ezekiel, amemshukuru Diwani Soko kwa msaada huo, akisema mashine hiyo itawarahisishia walimu kazi na kupunguza gharama za kuchapisha mitihani.
Mwanafunzi mwingine Emanuel George amesema mashine hiyo itasaidia kuhakikisha mitihani inachapishwa kwa usalama na kwa wakati, jambo litakaloweza kuchangia katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Emanuel ameomba wadau wa elimu kusaidia katika sekta ya michezo, ikieleza kuwa inakabiliwa na changamoto ya kukosekana vifaa vya michezo ikiwemo jezi, mipira na eneo linalofaa kwa michezo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo Sokola Patrirobas Privatus amempongeza Diwani wa eneo hilo kwa juhudi na moyo wa kujitolea katika kuboresha elimu, akisema hatua anazochukua zimekuwa mfano wa kuigwa ndani ya Manispaa ya Kahama.
Mwenyekiti huyo amesema Diwani amekuwa akitoa mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya shule na kuinua kiwango cha elimu, akisisitiza kuwa hatua hiyo si mara yake ya kwanza, kwani awali alishiriki katika kusaidia upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi na sasa ameendelea kuelekeza nguvu katika elimu.
Amesema uwekezaji katika chakula na elimu una uhusiano mkubwa, kwa kuwa mwanafunzi anayepata chakula anakuwa na uwezo mzuri zaidi wa kujifunza.
Aidha, amewapongeza walimu wa shule hiyo kwa kujituma katika kutekeleza majukumu yao, akisema jitihada za viongozi na wadau wa elimu haziwezi kuwa na matokeo bila ushirikiano na uwajibikaji wa walimu.
Mwenyekiti huyo pia amesisitiza umuhimu wa elimu ya dini na malezi ya maadili kwa wanafunzi, akipendekeza walimu wa dini mbalimbali wanaohudumia shule hizo kushirikishwa na kuwezeshwa ili kuimarisha malezi ya watoto.
Amesema elimu inapaswa kwenda sambamba na maadili na malezi bora, akieleza kuwa uwepo wa misingi ya kiroho na maadili unaweza kusaidia kujenga kizazi chenye nidhamu, hofu ya Mungu na uwajibikaji katika jamii.









No comments:
Post a Comment