Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba–Desemba 2026), ikionya kuwa msimu huo utaathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa iliyotokana na joto la bahari kuwa juu ya wastani katika Bahari ya Pasifiki.
Hali hiyo inatarajiwa kuchochea ongezeko la mvua za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Ziwa Viktoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.
Akizungumza kuhusu utabiri huo leo Agosti 18, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema msimu wa mvua za Vuli 2026 unatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa.
Aisha mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Ziwa Viktoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.
Dkt. Chang’a amesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba 2026 katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Viktoria, kabla ya kusambaa taratibu katika maeneo mengine mwezi Oktoba.
Amefafanua kuwa, ingawa kwa kawaida mvua za Vuli huisha mwezi Desemba, katika msimu wa Vuli 2026 mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kuendelea hadi Januari 2027, huku ongezeko kubwa la mvua likitarajiwa hasa mwezi Novemba 2026.
Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a amesema vipindi vya unyevu wa udongo kuzidi kiwango pamoja na mafuriko vinaweza kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo.
Pia amesema ongezeko la kina cha maji katika mabwawa na mito linaweza kuathiri miundombinu ya rasilimali za maji na nishati, huku magonjwa ya mlipuko yakijitokeza kutokana na uchafuzi wa maji.
Aidha, magonjwa ya mazao yanayosababishwa na kuvu, bakteria na virusi yanaweza kuathiri uzalishaji wa viazi mviringo, alizeti, maharage, ufuta, matunda na mbogamboga.
"Sekta za usafiri, ujenzi na utalii pia zinatarajiwa kukumbwa na changamoto za mmomonyoko wa barabara, uharibifu wa madaraja na kuhama kwa wanyamapori kutokana na mafuriko".
Dkt. Chang’a amewashauri wadau wa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kupanga na kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia taarifa mahususi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA, ikiwemo kuvuna maji ya mvua, kuimarisha miundombinu, kutoa tahadhari za mapema na kudhibiti mazalia ya mbu ili kupunguza magonjwa ya mlipuko.



No comments:
Post a Comment