Serikali inaendelea kuimarisha elimu, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuwawezesha Watanzania kupunguza utegemezi wa teknolojia na wataalamu kutoka nje ya nchi na kuchochea maendeleo ya taifa.
Kauli hiyo imetolewa Agosti 18, 2026 jijini Tanga na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, wakati akizindua Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, akieleza kuwa Tanzania inahitaji kuongeza uwezo wa wataalamu wake kubuni na kutumia teknolojia za kisasa zinazokidhi mahitaji ya ndani.
Amesema hatua hiyo inaweza kufanikiwa kwa kuwekeza zaidi katika sekta hiyo, kwani tayari Tanzania ina wataalamu wenye uwezo mkubwa wanaohitaji mazingira na fursa za kutumia maarifa yao kutengeneza bidhaa na huduma zenye tija kwa Taifa.
Waziri Mkenda amebainisha kuwa, Serikali imeendelea kuwekeza katika taasisi za elimu na mafunzo ya sayansi, teknolojia na ujuzi, sambamba na kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, ili kuongeza wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika uchumi wa kisasa.
Amesisitiza utafiti na ubunifu kuelekezwa katika kupata suluhisho za changamoto za wananchi, katika kilimo, afya, uzalishaji na mazingira. Sambamba na matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira na yanayolinda mahitaji ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha, amezitaka taasisi za elimu, watafiti, wabunifu, vijana na wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali kujenga Tanzania inayojitegemea kupitia elimu, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu, ili Taifa liweze kuzalisha wataalamu, bidhaa na teknolojia zenye ushindani ndani na nje ya nchi.𝗨𝗕𝗨𝗡𝗜𝗙𝗨, 𝗧𝗘𝗞𝗡𝗢𝗟𝗢𝗝𝗜𝗔 𝗦𝗜𝗟𝗔𝗛𝗔 𝗬𝗔 𝗧𝗔𝗡𝗭𝗔𝗡𝗜𝗔 𝗞𝗨𝗝𝗜𝗧𝗘𝗚𝗘𝗠𝗘𝗔 - 𝗣𝗥𝗢𝗙. 𝗠𝗞𝗘𝗡𝗗𝗔







No comments:
Post a Comment