UBALOZI WA MAREKANI WAAHIDI KUIMARISHA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, July 1, 2025

UBALOZI WA MAREKANI WAAHIDI KUIMARISHA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI NCHINI


Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umeeleza dhamira yake ya kusaidia kuimarisha misingi ya demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania, hayo yamejiri wakati kaimu balozi wa Marekani Andrew Lentz alipotembelea Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo, Kaimu balozi alifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC Bw. Kenneth Simbaya, waandishi wa habari kutoka Klabu ya Waandishi wa habari Dodoma, pamoja na wafanyakazi wa UTPC. Mazungumzo yalijikita kujadili mkwamo wa vyombo vya habari na njia madhubuti kukabiliana na changamoto hizo ili kuchochea maendeleo kijamii, kiuchumi na demokrasia.

Kaimu balozi Lentz alisistiza umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari katika jamii inayoheshimu demokrasia. Aliongeza kuwa ipo haja ya kusaidia taasisi za kihabari ili kulinda uhuru wa habari, aidha alibainisha kuwa ni lazima kuwasaidia Waandishi wa habari kufichua ukweli bila woga au vitisho kwa maslahi ya umma.

“Kutokana na umuhimu wa kazi yenu (waandishi wa habari) ya kufichua ukweli, lazima kuwepo na mazingira wezeshi ikiwemo sheria ili kuwasadia kufanya kazi zenu bila kuingiliwa na dola au wadau wengine” alisema Lentz.

“Uwepo wenu ni muhimu sana katika kuhabarisha Watanzania kuhusu maendeleo yao katika nyanja ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Kenneth Simbaya Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC , alitoa pongezi kwa ubalozi wa Marekani kwa utayari wao katika kusaidia waandishi wa habari nchini, aidha alitaja maeneo ya kipaumbele yanayohitaji msaada wa haraka kuwa ni pamoja na:-

Ulinzi na Usalama wa waandishi wa habari, msaada wa kisheria pindi anapokumbwa na changamoto kisheria, msaada wa matibabu pindi anapopata madhara ya kimwili na ulinzi dhidi ya vitisho vya kudhuru mwili, na vitisho vya mitandaoni.

Aliongeza kuwa msaada mwingine wa haraka ni mafunzo maalumu yatakayosaidia kuongeza uelewa wa sheria mbalimbali zinazohusu vyombo vya habari na utangazaji, kuongeza uelewa wa haki za vyombo vya habari na waandishi wa habari ili kuchochea upatikanaji wa habari kwa umma.

Pia, Simbaya alitoa shukrani kwa msaada wa awali uliotolewa na Ubalozi wa Marekani kupitia Mradi wa Uandishi wa Habari wa Maudhui Mbalimbali (Multicontent Journalism Program), ambao ulitekelezwa katika klabu 5 tu kati ya 28 za UTPC. Alisisitiza kuwa kutokana na maendeleo ya teknolojia ya habari, kuna umuhimu mkubwa wa kupanua mradi huo ili kuwajengea uwezo waandishi wa habari katika Klabu zote.

UTPC ni taasisi yenye mtandao mkubwa wa waandishi wa habari walioenea kote nchini kupitia Klabu za waandishi wa habari zinazopatikana mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar, mpaka sasa ina jumla ya Waandishi wa habari wanachama zaidi ya 1,500.

No comments:

Post a Comment