UZALISHAJI WA MADINI GEITA WAFIKIA TANI 27.43, MCHANGO WA SEKTA YA MADINI WAIMARIKA – RC SHIGELA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, July 21, 2025

UZALISHAJI WA MADINI GEITA WAFIKIA TANI 27.43, MCHANGO WA SEKTA YA MADINI WAIMARIKA – RC SHIGELA




Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigela, amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, sekta ya madini mkoani humo imepata mafanikio makubwa, ikiwemo ongezeko la uzalishaji wa madini kutoka tani 18.21 mwaka 2021 hadi kufikia tani 27.43 mwaka 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mhe. Shigela alisema kuwa mafanikio hayo yamechochewa na sera thabiti na mazingira rafiki ya uwekezaji yaliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

"Serikali ya awamu ya sita inatambua kuwa sekta ya madini ina nafasi ya kipekee katika kuchangia ukuaji wa Pato la Taifa, kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla," alisema.

Aidha, alieleza kuwa thamani ya fedha za kigeni zilizopatikana kupitia mauzo ya madini kutoka mkoani Geita imeongezeka kutoka Dola za Marekani 72,878,325.91 mwaka 2021 hadi Dola 92,204,527.35 mwaka 2025.

Kwa upande wa utoaji wa leseni kwa wachimbaji wadogo, Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa idadi ya leseni imeongezeka kutoka 903 mwaka 2021 hadi kufikia leseni 9,774 mwaka 2025, hatua inayochangia kuhamasisha uchumi shirikishi na ushiriki wa wananchi katika sekta ya madini.

Katika hatua nyingine, Mhe. Shigela alieleza kuwa Mkoa wa Geita umepokea zaidi ya Shilingi trilioni moja kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, miundombinu, maji, nishati, kilimo, mifugo, uvuvi, misitu, utalii, viwanda, biashara, uwezeshaji wananchi kiuchumi pamoja na miradi ya kimkakati.

Akielezea mafanikio katika sekta ya afya, alisema kuwa kumekuwa na uboreshaji mkubwa wa miundombinu ya kutolea huduma, ongezeko la upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, pamoja na huduma bora za afya kufikishwa karibu zaidi na wananchi.

No comments:

Post a Comment