
Na Meleka Kulwa -DODOMA
Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, viongozi wa dini wameendelea kutoa wito kwa Watanzania kudumisha amani, wakisisitiza umuhimu wa maadili, mshikamano na matumizi ya kauli njema katika kipindi hiki nyeti kwa mustakabali wa taifa.
Akizungumza Julai 8, 2025, Jijini Dodoma, Mchungaji Meshack Tulana Nhuti kutoka Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Central Tanganyika, Parishi ya Nhalawanda Nzuguni B – Kanisa la St. John, amesema kuwa kanisa lina jukumu kubwa la kuhubiri na kudumisha amani miongoni mwa waumini na jamii kwa ujumla.
"Sisi kama kanisa tunahubiri amani. Pale tunapokosa kuhubiri amani, machafuko yanaweza kuingia. Hivyo basi, tuhubiri amani katika kila hatua na kwa kila mtu," amesema Mchungaji Meshack.
Amesisitiza kuwa kila kiongozi wa dini anapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kulinda amani ya taifa.
"Sote ni wahubiri wa amani, iwe ni Kanisa Katoliki, Anglikana au makanisa ya Kipentekoste. Tunapaswa kuhubiri maneno yanayojenga na sio kubomoa," amesisitiza.
Akizungumzia nafasi ya dini katika kulinda amani, Pastor Meshack amesema taasisi za kidini ni sauti kuu katika jamii, hivyo viongozi wake wana ushawishi mkubwa kwa waumini wao.
"Ukihubiri chuki, watu watafuata chuki. Ukihubiri amani, watu wataenenda kwa amani. Tunapaswa kuwa na maadili, utu na kumcha Mungu," amesema.
Katika kuelekea uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais, Pastor Meshack amewahimiza Watanzania waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpiga Kura kujitokeza kwa wingi na kutimiza haki yao ya msingi ya kupiga kura.
"Kura ni haki yako ya msingi. Tumia kura yako kuwachagua viongozi unaowaamini. Na kwa wale walioamua kugombea, tunawaombea na kuwasihi kutumia lugha nzuri katika kampeni. Lugha ya matusi au kashfa haitujengi, bali inabomoa taifa," amesema.
Aidha, amewahimiza vijana kutumia nafasi zao kikamilifu katika ujenzi wa taifa na kanisa, akisisitiza kuwa taifa linawategemea.
"Nawatakia uchaguzi wenye amani, furaha na upendo. Tuwe na Tanzania mpya yenye mshikamano," amesema kwa matumaini.
No comments:
Post a Comment