KASI NDOGO YA UTEKELEZAJI MRADI WA UMEME WA CHALINZE- DODOMA YAMKASIRISHA DKT. BITEKO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, August 20, 2025

KASI NDOGO YA UTEKELEZAJI MRADI WA UMEME WA CHALINZE- DODOMA YAMKASIRISHA DKT. BITEKO



Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekagua
mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400 kutoka
Chalinze hadi Zuzu Dodoma na kueleza kutoridhishwa kwake na
utekelezaji wa mradi huo ambao ulipaswa kuwa umefikia asilimia 31
lakini kwa sasa umefikia asilimia 24 tangu kuzinduliwa kwake Novemba
mwaka 2024.

Hali ya kusuasua kwa mradi imebainika wakati Dkt. Biteko akikagua
mradi huo katika Kijiji cha Manchali wilayani Chamwino mkoani Dodoma
tarehe 20 Agosti 2025 ambapo Dkt. Biteko amemuagiza mkandarasi kampuni
ya TBEA ya China kuhakikisha kuwa anafidia muda wa kazi uliopotezwa wa
asilimia Saba ili mradi ukamilike kwa wakati kutokana na umuhimu wake
nchini.

Mwezi Novemba, 2024 Serikali ilikubaliana na mkandarasi kuwa mradi huo
ufanyike ndani ya miezi 19 tu badala ya miezi 22 kwani wakati mradi
unazinduliwa tayari kazi kubwa za awali zilikuwa zimeshafanyika
ikiwemo za upembuzi yakinifu na utoaji wa maeneo.

“ Leo ni miezi saba imepita tangu tuzindue mradi sawa na asilimia 32
ya muda wote tuliokuwa tunahitaji kutekeleza mradi huu, na
tulitegemea mradi kwa sasa ufikie asilimia 31 lakini katika hali ya
kushangaza mradi umefikia asilimia 24 tu jambo ambalo halikubaliki.”
Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko ameeleza kuwa, sababu zilizotolewa na Mkandarasi za
kuchelewesha mradi ikiwemo ya wananchi kugoma kutoa maeneo kwa madai
ya fidia na kukutana na miamba katika mkuza wa mradi hazikubaliki
kwani wananchi hao wana haki na lazima walipwe fidia.

Kutokana na hali hiyo, ameagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
kutumia mapato yake ya ndani kulipa fidia wananchi waliopisha mradi.

Dkt. Biteko ametanabaisha kuwa mkandarasi alishaagizwa asiutekeleze
mradi huo kwa mazoea kutokana na umuhimu wake kwani kwa sasa
miundombinu inayosafirisha umeme kwenda Dodoma kutoka mradi wa Julius
Nyerere (JNHPP) kupitia kituo cha Chalinze inabeba umeme kidogo kwa
takriban megawati 240 tu ambayo ni sawa na mashine moja tu kati ya
mashine 9 za JNHPP hivyo njia hiyo mpya ya umeme ya kV 400 inayojengwa
ni muhimu.

Amesisitiza kuwa njia mpya ya umeme ya kV 400 ni muhimu kwani katika
Mkoa wa Dodoma mahitaji ya umeme yanaongezka kila siku huku mkoa huo
pia ukiwa ni kitovu cha usambazaji umeme katika mikoa yote ya
Magharibi ikiwemo Singida, Tabora, Shinyanga Mara na Kigoma ambayo
inategemea utulivu wa umeme katika Mkoa wa huo na kwamba Rais, Dkt.
Samia Suluhu Hassan alishaagiza kuwa mradi huo usichezewe hivyo
Mkandarasi ahakikishe kuwa anaupa umakini mkubwa.

Kutokana na mradi huo kuwa nyuma katika utekelezaji, Dkt. Biteko
amemuagiza Mkandarasi kuja na mpango mpya wa utekelezaji wa kazi
ukiwemo wa kufidia muda uliopotezwa ambapo ametoa siku nne mpango wa
fidia ya muda uwasilishwe kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati.

Vilevile, Dkt. Biteko ameagiza mkandarasi kuongeza nguvu kazi ya watu
ili minara 917 ya umeme inayopaswa kujengwa kwenye mradi huo ijengwe
kwani kwa sasa mkandarasi amechimba takriban mashimo 100 tu kwa ajili
ya usimikaji wa minara. Pia amemtaka Mhandisi mshauri wa mradi
kuhakikisha anasimamia mradi huo kwa ufanisi na aeleze ukweli pale
anapoona kuwa hauendi sawa.

Aidha amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, kutengeneza timu
itakayoungana na TANESCO kuusimamia mradi huo na kila wiki taarifa
itolewe kuwa umefikia wapi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaasa Wananchi kutozuia
utekelezaji wa miradi pale inapopita kwenye maeneo yao na Serikali kwa
upande wake itahakikisha kuwa wanapata haki wanazostahili kwani Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaelekeza kuwa hataki wananchi wafanyiwe
dhuluma ambapo wasaidizi wake wanahakikisha kuwa agizo hilo
linatekelezwa.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema mradi huo wa
usafirishaji umeme wa kV 400 kunaenda kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha
usambazaji umeme nchini.

Aidha, ameahidi kuyasimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Dkt. Biteko
ya kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati ili kuwezesha
umeme huo utakaofikishwa Dodoma, kusambazwa pia kwenye maeneo mengine
nchini.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa
TANESCO, Lazaro Twange amesema Mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa
msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma unakusudia
kusafirisha umeme wote unaozalishwa kutoka katika Bwawa la kuzalisha
umeme la Julius Nyerere (Megawati 2,115) na kuingiza kwenye gridi ya
Taifa kisha kuufikisha kwenye maeneo yote yenye mahitaji ya umeme.

Amesema mkataba na mkandarasi kampuni ya TBEA ulisainiwa mwaka 2024 na
mradi kuanza kutekelezwa mwezi Novemba 2024 ambapo mkandarasi
ameshalipwa awamu ya kwanza ya malipo ambayo ni shilingi za kitanzania
bilioni 107 na mhandisi mshauri ameshalipwa asilimia 15 ya malipo
yake.

Ameeleza kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri
wa Nishati yatafanyiwa kazi ikiwemo ya kuhakikisha kuwa mradi
unakamilika mwezi Juni au kabla ya Juni 2026 kwa mujibu wa mkataba.

Aidha, Ameishukuru Serikali chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kutoa shilingi bilioni 513 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo
ambao utakuwa na urefu wa kilometa 345 na kuhusisha minara ya umeme
ipatayo 917 kutoka Chalinze mkoani Pwani hadi Zuzu mkoani Dodoma.






No comments:

Post a Comment