MRADI WA TACTIC KUBADILISHA MANDHARI YA JIJI LA DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, August 25, 2025

MRADI WA TACTIC KUBADILISHA MANDHARI YA JIJI LA DODOMA




Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Dodoma, Dkt. Fredrick Sagamiko ameeleza kuwa ujio wa mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) umekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto mbalimbali katika jiji hilo.

Akiongea katika mahojiano maalum kiongozi huyo amebainisha kuwa miongoni mwa miundombinu inayojengwa ni pamoja na barabara zenye urefu wa kilomita 10.19 ambazo zitasaidia wananchi kufika maeneo ya huduma mbalimbali kwa urahisi na kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji.

Aidha ameeleza kuwa kupitia mradi huo, tayari ujenzi wa Soko la majengo unaendelea na kwamba hapo awali wafanyabiashara walifanya kazi zao katika mazingira magumu lakini kwa ujio wa mradi huo sasa watapata soko la kisasa lenye huduma mbalimbali ikiwemo maegesho ya magari na kwamba hata idadi ya wafanyabiashara itaongezeka na kufika jumla ya watu 875.

"Ujio wa mradi huu katika jiji letu ni ukombozi tosha kwa wananchi maana hali ya soko la majengo ilikuwa haiendani na hadhi ya Dodoma lakini sasa tunaenda kupata soko jipya", amesema Dkt Sagamiko.

Kuhusu maeneo mengine yatakayonufaika na mradi huo, kiongozi huyo amebainisha kuwa kuna ujenzi wa mitaro ya maji katika eneo la Ilazo, ujenzi wa stendi ya Daladala katika eneo la Nzuguni na Mnada mpya, huku akibainisha kuwa eneo la Nzuguni lina idadi ya watu wengi ambapo stendi ya Daladala inatakiwa.

Kwaupande wake, Bi. Rozy Mtundu ambaye ni mfanyabiashara katika soko la majengo amesema kuwa ujenzi wa soko hilo utasaidia kukuza uchumi wao kwani watafanya biashara katika mazingira ya kisasa.

Bw. Laurent Munish ambaye pia ni mfanyabiashara katika soko hilo ameipongeza Serikali kwa utatuzi wa changamoto zilizokuwepo kwa kipindi kirefu na kusababisha kero kwa wafanyabiashara ambazo zinaenda kuondolewa baada ya kukamilika kwa soko jipya.

Akielezea kuhusu ujenzi wa barabara ya Mkalama, Bw. Hamza Zuberi ambaye ni mkazi wa Mkalama ameipongeza serikali kwa kuleta mradi huo ambao utasaidia kuongeza thamani ya maeneo hayo na kurahisisha huduma ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi.



No comments:

Post a Comment