RAIS Samia Suluhu Hassan amepewa tuzo maalumu na wakandarasi nchini kwa kuthamini mchango wake na hatua alizochukua kwenye sekta ya ujenzi tangu aingie madarakani miaka minne iliyopita.
Rais Samia alipewa tuzo hiyo ambayo ilipokewa kwa niaba yake na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, katika tukio lililofanyika katika ukumbi wa The Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika tukio hilo, Waziri Ulega alisema uamuzi wa kumpa tuzo Rais Samia ni stahiki kwa sababu mambo ambayo ameyafanya kwenye wakati wake wa urais si siri na yanaonekana.
Akizungumza kwa kutoa mifano, Ulega alizungumzia ujenzi mkubwa wa barabara na madaraja ambao umefanyika katika kipindi cha miaka minne iliyopita, akisema ni kiwango cha rekodi.
“ Wakati mwingine sisi ambao tunaishi Tanzania hatuoni au tunaweza kubeza kile kilichofanyika. Lakini juzi hapa, Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, amesema siku hizi anapotea akija Dar es Salaam kwa sababu ya mabadiliko makubwa ya kimiundombinu yanayoendelea.
“ Kigoma zamani kulikuwa mbali sana lakini sasa kuiunganisha Kigoma na Tanzania zimebaki kilomita kama saba tu. Madaraja mengi yamejengwa ndani ya awamu ya kwanza kuliko katika awamu moja nyingine yoyote katika historia yetu,” amesema Waziri Ulega.
Kuhusu uwezeshaji wa wakandarasi wazawa, Ulega aliwaambia wakandarasi kwamba kitendo cha serikali ya Rais Samia kuongeza wigo wa kupata miradi ya ujenzi ambapo sasa wazawa wanapewa upendeleo kwa miradi ambayo thamani yake haizidi shilingi bilioni 50, kimeonyesha pia kwamba serikali inatamani kuona wazawa wakipata kazi zaidi.
Kuhusu mchango wa sekta ya ujenzi nchini, Ulega alisema sasa imekuwa mojawapo ya misingi muhimu ya maendeleo ya nchi ikichangia asilimia 16 ya Pato la Taifa huku takribani ajira milioni 1.8 zikizalishwa kupitia sekta hiyo.
Wakati huohuo, Ulega ametoa maagizo kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Musonde, na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mohamed Besta, kukaa na wataalamu na kutoa mapendekezo kwake kuhusu hatua za kuchukua ili kupunguza foleni katika eneo la Kamata na Buguruni jijini Dar es Salaam.
Ulega alisema maeneo hayo mawili yamekuwa mojawapo ya chanzo kikubwa cha foleni katikati ya jiji na kusema kukamilika kwa ripoti hiyo kutaifanya serikali ichukua hatua za haraka ili kuondokana na hali hiyo.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Chemba ya Wakandarasi na Miundombinu (CCIZ), Steven Mkomwa, alisema sekta hiyo imepata maendeleo makubwa katika miaka ya karibuni ingawa kuna changamoto zinahitaji kufanyiwa kazi
No comments:
Post a Comment