REA KUSAMBAZA MAJIKO BANIFU 10,650 MKOANI PWANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, August 18, 2025

REA KUSAMBAZA MAJIKO BANIFU 10,650 MKOANI PWANI



Na Mwandishi Wetu, Pwani


Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imetoa jumla ya Majiko Banifu 10,650 Mkoani Pwani ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za Serikali za kuhakikisha kila mwananchi anatumia Nishati Safi ya kupikia nchini.

Akizungumza leo tarehe 18 Agosti, 2025 ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Meneja wa Teknolojia za Nishati kutoka REA, Mha. Michael Kyessi amesema mradi huo unalenga kuuza na kusambaza Majiko Banifu kwa bei ya ruzuku ambapo mwananchi atachangia asilimia ishirini (20%) za gharama ya jiko huku asilimia themanini (80%) zikitolewa na Serikali.

“Mwananchi wa kawaida atachangia 20% tu za gharama za jiko ambapo bei ya jiko ni 56,000 na mwananchi atagharamika kuchangia shilingi 11,200 tu baada ya ruzuku kutolewa na Serikali” amesema Mha. Kyessi.

Sambamba na hilo Mha. Kyessi amebainisha thamani ya mradi huo kwa ujumla ni milioni 596,400,00 ambapo Serikali kupitia REA imetoa ruzuku ya shilingi milioni 477,120,00 ambayo ni sawa na asilimia themanini.

Katika hatua nyingine, REA inatekeleza lengo la Serikali ya Tanzania kufikia mpango wa Umoja wa Mataifa wa "Nishati Endelevu kwa Wote" (SE4ALL) wa upatikanaji wa nishati kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2030. Mradi huu utatumia nishati Jadidifu ili kuweza kufikia wananchi wa maeneo ya visiwani na utekelezaji wake ni kwa kupitia mradi wa Ufadhili unaotegemea Matokeo (RBF) kupitia Benki ya Dunia.
"Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kufunga mifumo ya umeme jua maeneo ya visiwani kwa
kutoa ruzuku kwa bei ya mwisho ya mtumiaji wa mfumo wa Umeme Jua ili kufanikisha upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo yaliyo mbali na Gridi ya Taifa, " Amesema Mha. Kyessi.

Mha. Kyessi amesema katika Mkoa wa Pwani mradi wa umeme jua unategemea kuhudumia visiwa 13 na jumla ya watoa huduma wawili (2) wanategemea kuhudumia visiwa hivyo kupeleka jumla ya mifumo 2,243 ndani ya kipindi cha miaka miwili (2) na gharama za mradi kwa mkoa wa Pwani ni shilingi bilioni 1.372 ambapo ruzuku ni shilingi milioni 935.7 sawa na asilimia 69 ya gharama zote ya mradi na shilingi milioni 436.6 ni fedha toka kwa wanufaika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge ameipongeza REA kwa mkakati wa kuendelea kuongeza matumizi ya Nishati safi na kuondoa kero kwa wananchi kuhusu matumizi ya kuni na mkaa ambayo ni hatarishi kwa afya zao.

Mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miezi 15 katika mkoa wa Pwani na jumla ya Majiko Banifu 10,650 yatasambazwa kwa wananchi.



No comments:

Post a Comment