TANZANIA, BURUNDI ZAZINDUA UJENZI WA RELI YA SGR UVINZA-MUSONGATI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, August 16, 2025

TANZANIA, BURUNDI ZAZINDUA UJENZI WA RELI YA SGR UVINZA-MUSONGATI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo (Jumamosi, Agosti 16, 2025) ameshiriki uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa ya kutoka Uvinza hadi Musongati na kuwahahikishia Watanzania na WanaBurundi kwamba ujenzi huo utaanza katika muda uliopangwa.

Waziri Mkuu ambaye ameshiriki hafla hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema reli hiyo itakayokuwa na urefu wa km.240 pindi  ikikamilika, itakuwa ndiyo reli ya kwanza inayounganisha nchi na nchi katika ukanda wa Afrika Mashariki. 

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika eneo la Musongati, Burundi,  Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo kutasaidia kuunganisha masoko na kuendeleza biashara baina ya Tanzania na Burundi. 

"Reli ikikamilika itafungua fursa kwa wananchi wetu ambao wataweza kutoka hapa hadi Dar es Salaam ndani ya siku moja. Hata kwenye usafirishaji wa mizigo, hivi sasa, lori linatumia saa 96 kutoka Dar hadi Bujumbura lakini baada ya kukamilisha ujenzi, usafirishaji wa mizigo kwa kutumia treni utatumia saa 20 tu."

"Mradi wa reli ya kisasa siyo tu kwamba utarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, bali pia utafungua milango ya fursa mpya za uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Burundi."

Akielezea kuhusu mradi huo, Waziri Mkuu amesema ujenzi wa reli hiyo utagharimu dola za Marekani bilioni 2.154 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitano na  kwamba mwaka mmoja baada ya ujenzi utakuwa ni wa matazamio. 

Kwa upande wake, Rais wa Burundi,  Meja Jenerali Evarist Ndayishimiye alisema kuanza kwa ujenzi wa reli hiyo kutatibu shauku ya muda mrefu ya nchi hiyo kuwa na usafiri wa reli. 

"Leo ni siku ya furaha sana kwetu. Tumepata jawabu la tangu enzi na enzi. Mwaka 1921, mradi huu ulianzishwa na Wabelgiji kisha wakaja Wajerumani lakini wakashindwa. Leo hii Tanzania na Burundi tumeweza," alisema.

Alisema nchi yake imebarikiwa kuwa madini mengi na kuna wakati aliitisha kikao cha wawekezaji kutoka nchi kadhaa. "Wengi walivutiwa na wakataka kuwekeza mara moja, lakini wakaniuliza, tukianza kuchimba madini ya Nickel, tutayasafirishaje?"

"Hiyo changamoto ilitufanya tubungue bongo zetu na kutafuta suluhisho.  Tunaishukuru sana Serikali ya Tanzania kwa kukubali kuungana nasi ili tuanze mradi huu muhimu. Tukitoka hapa, tunataka reli iunganishe hadi Kindu, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Na baada ya hapo, tunataka reli yetu ifike Afrika Magharibi kwenye ufukwe wa bahari ya Atlantiki kwani tunaamini njia hiyo itaharakisha kuleta maendeleo."

Rais Ndayishimiye alimpongeza Rais Dkt. Samia kwa kufikia hatua kubwa za maendeleo. "Ukirudi nyumbani mwambie Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwamba tunampongeza sana kwa kuleta maendeleo ya haraka nchini Tanzania."

"Nimekaa Tanzania kwa muda mrefu lakini kwa sasa nikija naweza kupotea. Magomeni napajua, Tabata na Vingunguti napajua, Mwenge napajua, na Kinondoni nilishakaa; lakini kwa sababu ya maendeleo yaliyopatikana, naweza kupotea. Tunamshukuru kwa uongozi wake imara,"
Rais huyo alizungumza kwa Kiswahili na kuamsha shangwe miongoni mwa wananchi waliohudhuria tukio hilo. 

Mapema, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alisema utekelezaji wa mradi huo unaenda sambamba na Ajenda 63 ya Umoja wa Afrika ambayo inataka bara la Afrika liunganishwe kwa mtandao wa reli ya kisasa. 

Alisema mbali na kuziunganisha nchi hizo mbili, kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo, kutarahisisha kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo. "Hivi sasa, kontena moja la futi 20 linasafirishwa kwa gharama ya dola za Marekani 3,800 lakini reli ikikamilika, gharama itashuka hadi dola za Marekani 2,000.

Alisema faida nyingine itakayopatikana baada ya mradi huo kukamilika ni kuwezesha kusafirisha mizigo mingi kwa wakati mmoja. "Hivi sasa, mzigo unaosafirishwa kwa lori moja ni tani 30, lakini reli ikianza kazi, tutaweza kusafirisha tani 3,000 kwa wakati mmoja," alisema Waziri Mbarawa.

No comments:

Post a Comment