Tanzania Kutuma Wanamichezo 492 Kushiriki Mashindano ya FEASSA 2025 Kenya - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, August 10, 2025

Tanzania Kutuma Wanamichezo 492 Kushiriki Mashindano ya FEASSA 2025 Kenya



Na OR-TAMISEMI


Jumla ya wanafunzi 492, ambao ni wanamichezo wa shule za msingi na sekondari, wanatarajia kushiriki mashindano ya michezo ya wanafunzi wa shule za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA), yatakayofanyika kuanzia Agosti 12, 2025, mjini Kakamega, Kenya.

Kwa mujibu wa Mratibu wa mashindano hayo kwa upande wa Tanzania, Bw. George Mbijima, ambaye pia ni Afisa Michezo Mwandamizi na Mratibu wa mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, amesema idadi hiyo ni ongezeko la wanamichezo 128 ikilinganishwa na wanamichezo 364 walioshiriki FEASSA 2024 nchini Uganda.

Bw. Mbijima amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kushinda michezo mingi mwaka huu kutokana na maandalizi makubwa yaliyofanywa na namna walivyowezeshwa na Serikali katika nyanja zote, kuhakikisha wanapeperusha bendera ya taifa kwa heshima.

Ameongeza kuwa nchi tano za Afrika Mashariki zimethibitisha kushiriki, ambazo ni Tanzania, Uganda, Burundi, Rwanda na Kenya (mwenyeji), huku Ivory Coast ikithibitisha kushiriki kama mgeni mwalikwa.

Baadhi ya wanafunzi wanaotarajiwa kushiriki wamesema wameandaliwa vizuri kisaikolojia na kupatiwa mahitaji yao yote ya msingi, hivyo wameahidi kufanya vizuri kwenye mashindano hayo.

Kwa sasa, timu ya Tanzania ipo kambini katika Chuo cha Ualimu Tarime, mkoani Mara, ikiendelea na maandalizi ya michezo hiyo.




No comments:

Post a Comment