WAZIRI CHANA AELEKEZA JESHI LA UHIFADHI NA JESHI LA POLISI KUSHIRIKIANA KUTATUA CHANGAMOTO ZA UHIFADHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, August 10, 2025

WAZIRI CHANA AELEKEZA JESHI LA UHIFADHI NA JESHI LA POLISI KUSHIRIKIANA KUTATUA CHANGAMOTO ZA UHIFADHI



Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) ameelekeza Jeshi la Uhifadhi (JU) na Jeshi la Polisi (PT) kuendelea kushirikiana katika utatuzi wa changamoto zinazoikabili Sekta ya Maliasili na Utalii ikiwemo matukio ya ujangili na utoroshaji wa nyara za Serikali.

Ameyasema hayo Agosti 9, 2025 alipokuwa akifungua rasmi kikao kazi kilichoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kati ya Jeshi la Uhifadhi na Jeshi la Polisi kilichofanyika katika Hifadhi ya Ziwa Manyara, Mkoani Arusha.

“Pamoja na mafanikio hayo na ushirikiano uliopo baina ya majeshi yetu, zipo changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza na kuhitaji ushirikiano zaidi wa pamoja katika kuzitatua ikiwa ni pamoja na zile zinazowakumba maafisa na askari wetu pindi wanapotekeleza majukumu yao ya kupambana na majangili wa aina mbalimbali wa nyamapori, meno ya tembo, samaki na ulishaji wa mifugo ndani ya hifadhi” amesisitiza Mhe. Chana.

Aidha, Mhe. Chana ametaja matukio hususan ya mifugo kuingizwa katika maeneo ya hifadhi, ambapo mara kadhaa askari hao wamekuwa wakivamiwa na makundi ya wafugaji kuanzia watu 50 na kuendelea wakiwa na silaha za jadi kwa lengo la kushinikiza kurudishiwa mifugo yao.

Awali akimkaribisha Waziri Dkt. Chana, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Uhifadhi Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba ameahidi kusimamia utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa hususan uwepo wa vikao vya mashirikiano na Jeshi la Polisi katika ngazi mbalimbali ikiwemo Kanda.

Naye Kamishna wa Polisi Charles Mkumbo, kwa niaba ya Jeshi la Polisi ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa jitihada kubwa inazofanya katika kuimarisha mashirikiano, na kuahidi kuwa Jeshi hilo litaeendelea kushirikiana na Jeshi la Uhifadhi kikamilifu, katika ulinzi wa Maliasili kwa maslahi mapana ya taifa.

Pamoja na Makamanda wengine, kikao hicho kinashirikisha, Viongozi waandamizi Wizara ya Maliasili na Utalii, Makamishana wa Polisi watano, Makamanda wa Polisi wa Mkoa 17, wakuu wa taasisi za Jeshi la Uhifadhi pamoja na Mkamanda waandamizi wa Jeshi la Uhifadhi.




No comments:

Post a Comment