Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw. Joel Laurent, amewahakikishia wakulima upatikanaji wa mbolea kwa wakati kwa kuzingatia mahitaji ya msimu wa kilimo kwa mwaka 2025/2026.
Joel ametoa kauli hiyo leo alipofanya ziara katika Kijiji cha Mbolea kilichopo kwenye viwanja vya Maonesho ya Nanenane, Nzuguni mkoani Dodoma.
Amesema kuwa ili kuhakikisha mbolea zinafika kwa wakulima kwa urahisi, serikali inapanga bei za pembejeo hizo kwa kuzingatia umbali mkulima aliko na hivyo kuwapa motisha wasambazaji na mawakala wa mbolea kufikisha pembejeo hiyo maeneo ya pembezoni.
“Tunaendelea kuhakikisha kwamba mbolea zinapatikana kwa wakati na kwa bei himilivu inayozingatia umbali kutoka katika chanzo,” ameongeza Joel.
Katika kuimarisha uwekezaji wa viwanda vinavyozalisha mbolea nchini, Joel amesema, katika msimu wa kilimo wa 2025/26 serikali imepanga kufanikisha ununuzi na upatikanaji wa kiasi cha tani 200,000 za mbolea kutoka kwa wazalishaji wa ndani pamoja na tani 50,000 za Chokaa mazao na kuzisambaza kwa wakulima nchini
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo wa Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu, Dkt. Mshindo Msolla, amesema kuwa kampuni hiyo imejipanga kuongeza uzalishaji wa mbolea zinazozingatia mahitaji halisi ya udongo kwa kila eneo nchini, kufuatia matokeo ya tafiti walizozifanya wakati wa majaribio ya mbolea zao.
No comments:
Post a Comment