USHIRIKISHAJI JAMII KATIKA MATENGENEZO YA BARABARA UTAIPUNGUZIA SERIKALI GHARAMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, August 23, 2025

USHIRIKISHAJI JAMII KATIKA MATENGENEZO YA BARABARA UTAIPUNGUZIA SERIKALI GHARAMA



Na Mwandishi Wetu, Korogwe, Tanga


Ushirikishwaji wa vikundi vya kijamii katika matengenezo madogomadogo ya miundombinu ya barabara umetajwa kuwa suluhisho la kupunguza gharama kwa serikali na kuongeza uimara wa barabara nchini.

Mhandisi Ephrahim Kalunde kutoka mradi wa RISE-TARURA ameyasema hayo wakati wa mafunzo elekezi kwa vikundi 30 vya kijamii vya wilayani Korogwe mkoani Tanga vinavyojihusisha na matengenezo ya barabara.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanatolewa kupitia mradi wa Uboreshaji Barabara Vijijini na Ufunguaji wa Fursa za Kijamii na Kiuchumi (RISE), ambao pamoja na mambo mengine unahamasisha wananchi kushiriki katika matengenezo madogomadogo ya barabara pindi uharibifu unapotokea.

“Njia ya kutumia vikundi kufanya matengenezo ya barabara kwenye maeneo yao itasaidia serikali kupunguza gharama kwani matengenezo yatafanyika kwa wakati. Pia, itapunguza gharama za kumpata mkandarasi kwa kuwa shughuli hizi zinaweza kufanywa na wananchi waliopo kwenye eneo husika na kuhakikisha barabara zinapitika muda wote,” amesema Mhandisi Kalunde.

Ametaja baadhi ya kazi zitakazofanywa na vikundi hivyo kuwa ni pamoja na kukata nyasi, kusafisha mifereji ya barabara na kujenga miundombinu midogo midogo isiyohitaji vifaa vikubwa vya ujenzi.

Kwa mujibu wa Mhandisi Kalunde, kupitia mradi huo watafikia mikoa 25 ya Tanzania Bara na kwa awamu ya kwanza ambayo imeanza inahusisha mikoa minne na halmashauri za wilaya nane.

Naye, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka TARURA, Bw. Owigo Phinias amesema mafunzo hayo yatawajengea vikundi ujuzi wa kitaalamu hatua ambayo pia itawasaidia kujikwamua kiuchumi kupitia kazi za matengenezo ya barabara.






No comments:

Post a Comment