Na Okuly Julius, OKULY BLOG , Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Zuhura Yunus, amesisitiza umuhimu wa vijana kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kudumisha amani na usalama wa nchi.
Akizungumza leo jijini Dodoma katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa, Yunus amewataka vijana kote nchini kushiriki mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa amani na utulivu, akibainisha kuwa vitendo vya uvunjifu wa amani vinaweza kuhatarisha mustakabali wa taifa.
“Nitoe rai kwa vijana wote nchini kushiriki katika mchakato wote wa uchaguzi kwa amani na utulivu. Vijana mnatakiwa kuwa makini katika kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani,” amesema.
Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, msingi wa maendeleo ya taifa ni amani na usalama, huku vijana wakihesabika kama nguzo muhimu ya kulinda na kuendeleza utulivu uliopo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Suleiman Mvunye, amewataka vijana walioko vyuoni na waliomaliza elimu ya sekondari kuhakikisha wanajifunza stadi za maisha zitakazowawezesha kujipatia kipato halali na kujitegemea kiuchumi.
Mvunye amesema stadi za maisha kama ujasiriamali, ujuzi wa kiufundi na teknolojia ni nguzo muhimu kwa vijana kujikwamua kimaisha, huku akibainisha kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya vijana.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya maendeleo ya vijana,” amesema Mvunye.
Kwa upande wake, Meneja wa Miradi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Joseph Manirakiza, amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali katika kuwekeza kwa vijana kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
No comments:
Post a Comment