
Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, ameeleza kuwa jumla ya vitongoji 1,997 sawa na asilimia 88.4 kati ya vitongoji 2,260 vimeshapatiwa huduma ya umeme kupitia miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), iliyopita na inayoendelea kutekelezwa katika mkoa wa Kilimanjaro.
Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu amebainisha hayo leo Agosti 29, 2025 wakati wa ziara ya kutembelea utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, sambamba na kuzungumza na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA ambapo ameweza kushuhudia wananchi wakiunganishiwa huduma ya umeme Wilaya ya Hai mkoani humo.
"REA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika mkoa huu kwa kasi zaidi ukiwa na lengo la kuwapatia huduma za nishati wananchi wote ili kuboresha huduma za kijamii katika maeneo hayo ya vijijini," Amesema Mhe. Balozi Kingu.
Ameeleza kuwa, mkoa wa Kilimanjaro una jumla ya vijiji 519 ambapo vijiji vyote 519 sawa na asilimia 100 vimepata huduma ya umeme kupitia miradi ya REA iliyotekelezwa katika mkoa huo.
Kwa upande wake, Mhandisi Miradi wa REA mkoa wa Kilimanjaro Mha. Kelvin Melchiad, amesema kuwa REA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali mkoani humo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Wakala wa kufikisha umeme kwa wananchi wote nchini.
"Katika mkoa huu jumla ya miradi miwili ya kusambaza umeme vitongojini inatekelezwa ambayo ipo katika hatua za utekelezaji ukiwemo mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji (Hamlets Electrification Project HEP 2A), " Amesema Mha. Melchiad.
Halikadhalika, Serikali kupitia REA imetoa jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 32.7 ili kuhakikisha miradi ya umeme inatekelezwa mkoani humo na wananchi wanapatiwa huduma ya umeme ili kuwapatia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake, Diwani Mstaafu wa Kitongoji cha Lomate Elinisaah Kileo, amemshukuru Rais Samia kwa kuiwezesha REA kuweza kupeleka huduma ya umeme katika eneo hilo hali inayokwenda kuchochea maendeleo yao.




No comments:
Post a Comment