
Afisa kutoka Idara ya Uchambuzi wa Sera Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Fronto Furaha (kushoto), akitoa elimu kwa baadhi ya wakazi wa jiji la Dodoma, kuhusu ripoti ya hali ya Uchumi ya nchi mwaka 2024 kwa wakazi wwa jiji la Dodoma, walipofika kutembelea Banda la Wizara ya Fedha, kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo na Uvuvi 2025.




Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema (kulia), akikabidhiwa vipeperushi vya huduma zinazotolewa na Kitengo cha Mkataba cha Wizara hiyo na Mkutubi Mwandamizi wa kitengo hicho, Bw. Fredy Mpoma, wakati alipofika kutembelea Banda la Wizara ya Fedha, kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo na Uvuvi 2025.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
Na Josephine Majura na Joseph Mahumi, WF, Dodoma.
Wananchi wamehimizwa kufika kwa wingi katika Banda la Wizara ya Fedha kwenye Maonesho ya Kilimo (Nanenane) Kitaifa yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma, ili kupata elimu kuhusu misamaha ya kodi inayotolewa na Serikali katika Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kama chachu ya kukuza sekta hizo nchini.
Wito huo umetolewa na Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uchambuzi wa Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Fronto Furaha, alipokuwa akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea Banda hilo.
Alisema kuwa ni muhimu kwa wananchi wanaojihusisha na kilimo, ufugaji na uvuvi kufahamu haki na wajibu wao katika mfumo wa kodi, pamoja na kufahamu fursa ya misamaha mbalimbali ya kodi iliyotolewa katika kilimo, ufugaji na uvuvi.
“Tunaalika wananchi wote kutembelea Banda letu ili kupata uelewa mpana kuhusu aina mbalimbali za misamaha ya kodi inayotolewa, masharti ya kuipata, pamoja na taratibu sahihi za kunufaika na misamaha hiyo,” alisema Bw. Furaha.
Alibainisha kuwa lengo kuu la utoaji wa elimu hiyo ni kuwajengea wananchi uelewa wa kina juu ya nani anayestahili kupewa msamaha wa kodi, kwa nini misamaha hiyo hutolewa, na athari chanya inazozalisha katika uchumi na maendeleo ya kijamii.
“Kuna dhana potofu miongoni mwa baadhi ya wananchi kuwa misamaha ya kodi hutolewa kwa upendeleo au watu maalum tu, tunataka kuondoa dhana hiyo kwa kutoa elimu ya kina kuhusu vigezo vinavyotumika na namna ya kunufaika kupitia mifumo ya Serikali,” alifafanua Bw. Furaha.
Aidha, Bw. Furaha, alieleza kuwa misamaha hiyo inalenga kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi ambapo pembejeo na viuatilifu vya kilimo, vifaa vya uvuvi na mifugo vinavyoingizwa nchini kwa ajili ya sekta hizo, vinapewa misamaha kulingana na taratibu na sheria, ambapo misamaha hiyo imeendelea kuwa chachu kwa sekta hizo kuendelea kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii.
Aliainisha kwa mifano, baadhi ya pembejeo za kilimo, mitambo ya uchakataji wa mazao ya kilimo, viuatilifu vya kilimo, vifaa vinavyotumika katika uvuvi kama nyavu za uvuvi na vifaa vinavyotumika katika ufugaji vinapewa msamaha wa kodi kwa maendeleo ya sekta hizo, ambayo moja kwa moja yanagusa maisha ya wananchi wa kawaida.
Baadhi ya Wananchi waliotembelea Banda hilo walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, ambayo imewasaidia kuelewa zaidi kuhusu jinsi wanavyoweza kunufaika kisheria na misamaha ya kodi, na pia kuchangia katika kukuza uchumi wa Taifa kwa kufuata taratibu sahihi.
Wizara ya Fedha imeahidi kuendelea kushirikiana na wananchi kwa kutoa elimu kupitia maonesho, semina na mikutano ya hadhara, ili kuhakikisha wananchi wanakua na uelewa mpana wa masuala ya misamaha ya kodi.
Wizara ya Fedha pamoja na Taasisi zilizo chini yake inashiriki katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo na Uvuvi 2025’’.
No comments:
Post a Comment