Chama Cha Mapinduzi CCM kikiongozwa na Mgombea wake wa Urais wa Tanzania pamoja na wagombea Ubunge na Udiwani kwenye Mkoa wa Iringa wamedhamiria kuendelea kuboresha huduma muhimu za Kijamii katika miaka mitano ijayo ikiwa watapata ridhaa ya kuongoza katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kulingana na kitabu kidogo cha Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Chama hicho kwa Wilaya ya Iringa kimedhamiria kutekeleza Ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Iringa dc, kujenga vituo 7 vya afya na zahanati 15, ujenzi wa shule mpya 22 za msingi na sekondari, madarasa 495, maabara 30, majengo ya utawala 8, ujenzi miradi 11 ya maji, ukarabati wa mradi wa maji ya Magubike, Tungamalenga, Tanangozi- Kalenga na Malinzanga, Ujenzi wa skimu 3 za maji Ifunda- Ihemi- Weru, Kibebe na Ikungwe, Kuboresha huduma za ugani Iringa DC pamoja na kutekeleza Ujenzi wa ghala la kuhifadhia parachichi kwenye Kijiji cha Luhindo
Katika Manispaa ya Iringa ambapo Mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa na Mkutano wake wa kampeni mapema leo kwenye uwanja wa michezo wa Samora, CCM imeahidi kutekeleza ujenzi na ukarabati wa Hospitali ya Frelimo, Vituo vya afya na Zahanati, ujenzi wa shule 5 mpya za Msingi, madarasa 294, nyumba sita za waalimu, Ukarabati wa shule kongwe za sekondari, Uboreshaji wa huduma ya maji safi na Majitaka Manispaa ya Iringa, Kukamilisha machinjio ya kisasa ya Ngerewala, ujenzi wa majengo matatu ya kitega uchumi pamoja na kukarabati masoko 7 ya Halmashauri.
Kwa Wilaya ya Kilolo yenye Jimbo moja la Uchaguzi ,Chama Cha Mapinduzi CCM kimeahidi kufanya ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma, ujenzi wa shule mpya 20, madarasa 495, maabara 9, majengo ya TEHAMA 25, Nyumba za waalimu 45, ujenzi wa miradi 13 ya maji pamoja na ujenzi wa machinjio 5 za kisasa.
Aidha kwa Mji wa Mafinga Chama hicho pia kimedhamiria kutekeleza ujenzi na ukarabati wa Hospitali ya Mji Mafinga, ujenzi wa shule mpya ya English Medium, ujenzi wa madarasa 20, mabweni na mabwalo ya chakula kwenye shule za sekondari, ujenzi wa madarasa 132 pamoja na ujenzi wa nyumba 16 za waalimu wa shule za msingi
Kwa Wilaya nyingine ya Mufindi pamoja na mambo mengine, Chama hicho tawala tangu uhuru wa Tanzania kimeahidi pia ujenzi wa miradi 21 ya maji, kuanzisha mashamba darasa kwenye Vijiji pamoja na uanzishaji wa vituo vya kukusanya na kuuza maziwa, ukamilishaji wa barabara ya kiwango cha lami ya mtii- Ifwagi, Tanzam 1 pamoja na barabara ya Kasanga- Ihosa.
No comments:
Post a Comment