
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Watu Tisa wamepoteza maisha huku wengine 16 wakijeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi la Kampuni ya Babu Trans yenye namba T 129 DVX lililokuwa likitokea Wilaya ya Kondoa kuelekea Dodoma Mjini na Lori la mizigo lenye namba T 907 EGZ lililokuwa likitokea Dodoma Mjini kwenda Kondoa.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo leo Septemba 18,2025 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma SACP Gallus Hyera amesema ajali hiyo imetokea majira ya asubuhi saa Moja kasoro dakika 20 katika eneo la Kambi ya Nyasa Wilayani Chemba Mkoani Dodoma.
"Chanzo ambacho kimepelekea ajali hii kutokea kwa jinsi tulivyokagua eneo la tukio lakini na baadhi ya hata majeruhi walivyojaribu kuelezea kwa dereva wa Lori katika eneo la tukio alihama upande wake wa kushoto kuelekea upande wa kulia ambako aligongana uso kwa uso na dereva mwenzie yule wa gari la basi,"amesema.
SACP Hyera amesema katika ajali hiyo iliyoghalimu maisha ya watu Tisa dereva wa Lori ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa akiwa anaendelea na matibabu huku dereva wa basi akiwa amepoteza maisha papo kwa papo eneo la tukio.

Aidha, ametoa wito kwa madereva kuzingatia Sheria za usalama barabarani ili kuepukana na matukio kama hayo yanayoghalimu maisha ya watu.
"Matukio kama haya kwa uzembe kama hivi tunavyojaribu kuelezea umeghalimu maisha ya wenzetu Tisa, lakini pia kuna hawa wenzetu wanaendelea na matibabu, inaleta shida kwa familia ambao walijipanga kwa mambo mengine lakini sasa hivi wanahangaikia kunusuru maisha ya hawa wengine ambao wanaendelea na matibabu lakini pia kuwastili hawa wengine Tisa waliokutwa na mauti,"amesema.
Pia ametoa rai kwa madereva muda wote waendeshe kwa tahadhari.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Ibenzi Hernest amethibitisha kupokea majeruhi Tisa ambao kwasasa wanaendelea na matibabu katika jospitali hiyo.
"Asubuhi tulipata taarifa ya kutokea kwa ajali Wilayani Chemba lakini sisi kuanzia saa 4 asubuhi tukaanza kupokea majeruhi ambao mapaka sasa tumepokea majeruhi wako Tisa na wote wanaendelea na huduma, hao majeruhi wameumia sehemu mbalimbali za mwili, sisi madaktari na watumishi wote wa sekta ya afya kwa niaba ya Wizara ya Afya tutaendelea kuwatibu wagonjwa hawa wote na kuhakikisha wanapona,"amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ametoa pole kwa familia zilizopatwa na msiba huo.



No comments:
Post a Comment