CCM YAAHIDI UMEME, HUDUMA ZA AFYA NAMONGE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, September 18, 2025

CCM YAAHIDI UMEME, HUDUMA ZA AFYA NAMONGE



Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko amesema CCM imepanga kuongeza kasi ya maendeleo katika Kata ya Namonge kwa kusogesa karibu huduma za jamii.

Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 18, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Namonge wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

“ Hapa tuna vitongoji sita kati yake vitatu havina umeme, mkituchagua tutakamilisha umeme katika vitongoji vyote, tunataka kila nyumba iwe na umeme, amesema Dkt. Biteko

Akizungumzia huduma za afya amesema “ Nataka nimwambie Mtendaji wa Kata hii hatutaki vikao vya muda mrefu wananchi hawa wanahitaji huduma, nimenunua vifaa kwa ajili ya zahanati ningependa kuona imekamikika na inatoa huduma kwa wananchi ili wasitembee kilomita 12 kufuata huduma,”

Aidha, amesema Kata hiyo imepiga hatua kimaendeleo ambapo awali kulikuwa na shule saba za msingi na sasa zipo 14, kuna shule mbili za sekondari kutoka moja pamoja na kituo kikubwa cha afya ambacho upasuaji tayari umeanza kufanyika.

Dkt. Biteko ametaja mipango ya CCM kwa miaka mitano ijayo katika Kata hiyo kuwa ni kujenga shule katika maeneo yasiyo na huduma hiyo pamoja na kuongeza ujenzi wa zahanati Mji mwema na Bugega sambamba na kukamilisha zahanati ya Ilyamchele.

Ameendelea kusema kuwa maendeleo ya Namonge yametokana na upendo wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akitoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo hivyo amewahimiza wananchi hao kujitokeza kwa wingi na kumpigia kura ili aweze kuendeleza jitihada za maendeleo katika Kata yao.

Naye, Mgombea wa Udiwani Kata ya Namonge, Mlalu Bundala amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Dkt. Samia na Biteko wamesaidia kujenga daraja, Shule ya Msingi Ilyamchele, Shule ya Sekondari Said Mkumba pamoja na kujenga barabara ya Ilyamchele hadi Nyamagana.

Amesema kuwa mafanikio hayo yametokana na jitihada zao za kuwaletea maendeleo wananchi wa Namonge na hivyo Oktoba 29 mwaka huu wajitokeze kwa wingi na kuwapigia kura wagombea wa CCM.


Katika hatua nyingine, akizungumza na wananchi wakati akiendelea na kampeni katika Kata ya Bulega, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali inatekeleleza miradi ya maendeleo ikiwemo mradi wa maji, wamechimba visima vitano, kujenga zahanati pamoja na kupeleka umeme katika vijiji vyote.

Aidha, amesema wanahitaji kuongeza nguzo za umeme na kuwa wakichaguliwa Oktoba 29 watafanya hivyo ikiwa ni pamoja na kuendeleza programu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia wkatika Wilaya ya Bukombe.

“ Ni lazima tuongeze shule hapa ya kidato cha tano na sita ili watoto wanaotoka maeneo mengine pia wapate fursa ya kusoma hapa,” amesoma Dkt. Biteko.

Amesisitiza kuwa endapo wakichaguliwa tena watahakikisha wanajenga soko, barabara pamoja na kukarabati shule chakavu.

“ Dkt. Samia ametoa fedha ya kujenga barabara ya lami kutoka Ushirombo kwenda Katoro hadi Geita, nataka nimuombe tena fedha kwa ajili ya kujenga shule ya kidato cha tano na sita sasa ili kazi hii ifanyike nawaomba msiniangushe, Oktoba 29 mkampigie kura Dkt. Samia ,” amesema Dkt. Biteko

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Bulega, Erick Kagoma amesema kuwa kwa miaka 10 Kata hiyo imepiga hatua ya maendeleo kwa kutekeleza ilani ya CCM.

Ambapo wamejenga shule za msingi mpya tatu, wameongeza umeme kutoka vitongoji viwili hadi nane pamoja na kuboresha barabara kadhaa katika Kata hiyo.

“ Sasa tumekuja kwenu kuomba ridhaa ili mimi, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Biteko tuweze kutekeleza ilani ya CCM kwa kujenga shule, hospitali, kuweka umeme hivyo naomba mtuchagu,” amesema Kagoma.

No comments:

Post a Comment