DC NYAMWESE: BIL.1.3/- KULIPA FIDIA WANANCHI MRADI WA GRIDI IMARA HANDENI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 19, 2025

DC NYAMWESE: BIL.1.3/- KULIPA FIDIA WANANCHI MRADI WA GRIDI IMARA HANDENI



Na Mwandishi Wetu,Handeni


ULIPAJI fidia kwa wananchi waliopisha Mradi wa Gridi Imara umezinduliwa rasmi katika maeneo ya Mkata, Handeni na Kilindi, huku serikali imeahidi kulinda maslahi ya wananchi na kuhakikisha nishati bora inawanufaisha wote.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, akizindua zoezi hilo, amesema kiasi cha Sh.Bilioni 1.3 kitatumika kulipa fidia kwa wananchi hao na kueleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya kuthamini utu wa mwananchi na uwekezaji alioufanya.

Amesisitiza kuwa jukumu la wananchi sasa ni kulinda miundombinu ya umeme ili manufaa ya mradi huo yaendelee kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

“Fidia hii ni kielelezo cha kujali utu na mchango wa kila mmoja. Tukiharibu au kutoheshimu miundombinu hii, hasara kubwa itakuwa yetu sote,” amesema Nyamwese.

Kwa upande wake, Meneja wa mradi huo, Mhandisi Jafari Mpina, amesema serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mfumo wa umeme katika wilaya ya Handeni, hatua itakayochochea fursa za kiuchumi kwa wananchi, ikiwemo kuimarisha biashara na kuongeza ajira.

Naye, Meneja wa CRDB tawi la Handeni Carlos amebainisha kuwa malipo yote yatatolewa moja kwa moja kupitia akaunti binafsi za wanufaika, jambo linaloimarisha usalama wa fedha na kuondoa hofu ya upotevu.

Wananchi walionufaika na fidia hiyo wameishukuru serikali, wakieleza kuwa hatua hiyo imeimarisha maisha yao na kuwapa matumaini mapya ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

No comments:

Post a Comment