DKT. SAMIA AAHIDI KASI ZAIDI UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO KILIMANJARO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 30, 2025

DKT. SAMIA AAHIDI KASI ZAIDI UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO KILIMANJARO


Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kukamilisha miradi mikubwa ya maendeleo katika Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, akiahidi pia kwamba ndani ya Mwaka mmoja na nusu ujao umeme utakuwa umefika kwenye Vitongoji vyote vya Tanzania.

Akizungumza na wananchi wa Same leo Septemba 30, 2025 kwenye Viwanja vya Stendi ya Mabasi Same, Dkt. Samia amesema CCM imeweka kipaumbele cha kuimarisha huduma za jamii, miundombinu ya barabara, elimu, afya na maji, ili kuinua maisha ya wananchi wa wilaya hiyo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Dkt. Samia amebainisha kuwa tayari barabara za milimani zikiwemo Mwembe–Myamba–Ndungu, Lembeni–Kilomeni–Lomwe na Kifaru–Kirurumo–Kichwa cha Ng’ombe zimekamilika, sambamba na daraja la Hingiriri lililojengwa ili kurahisisha usafiri na shughuli za kibiashara. Aidha, amesema barabara ya Same–Kisiwani–Mkomazi nayo imefungua fursa kubwa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Katika sekta ya afya, Dkt. Samia ameahidi kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Same, huku barabara za lami zikijengwa katika mji wa Same na barabara za kiwango cha changarawe zikiboresha usafiri maeneo ya John Malecela, Makanya–Ruvu–Muungano, Same–Ruvu–Mferejini na Makuruvila.

Akizungumzia huduma za maji, amesema miradi ya Mroyo, Vuje, Kihurio, Msindo Awamu ya Pili na Maore–Beseline–Ihindi itakamilishwa, sambamba na ukarabati wa skimu za umwagiliaji katika maeneo ya Maore, Ngoja, Igoma, Kalemane, Bendera, Mbuyu na Yongoma, ili kuongeza uzalishaji wa kilimo.

Vilevile, ameeleza kuwa mradi mkubwa wa tangawizi “Mamba Myamba” wenye thamani ya Shilingi bilioni 2.5 ni kielelezo cha uwekezaji utakaosaidia wananchi kuongeza kipato, huku sekta ya elimu ikiboresha kupitia ujenzi wa shule mpya ikiwemo Sekondari ya Angellah Kairuki.

Katika sekta ya utalii, amesema Serikali yake itaendelea kuimarisha vivutio kwa kukamilisha jengo la kulia chakula katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi pamoja na kuchimba visima viwili vya maji kwa ajili ya wanyamapori.

No comments:

Post a Comment