
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumamosi Septemba 13, 2025 akiwa Kasulu Mjini Mkoani Kigoma kwenye muendelezo wa kampeni zake kuelekea Oktoba 29, 2025, ameahidi kukamilisha ujenzi wa barabara zote za Kasulu Mjini ili kuendelea kuvutia zaidi biashara na uwekezaji na kurahisisha shughuli za kiuchumi kupitia usafiri na usafirishaji.
Dkt. Samia wakati akizungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza, amezitaja barabara hizo kuwa ni za Manyovu- Kasulu Kilomita 68, Barabara ya Kanyani- Vugwe, Vugwe- Nduta pamoja na barabara ya Nduta- Kibondo, akisema kukamilika kwake kutaifanya Kigoma kuwa Miongoni mwa Mikoa yenye barabara nzuri za lami nchini.
Dkt. Samia pia ameahidi kuwa ikiwa atachaguliwa katika uchaguzi Mkuu ujao atajenga pia barabara ya Ilani- Mwanga- Muyama, Uvinza- Kanyani na Mugome- Kagera Nkanda Kilomita 36.
"Tunaamini kwamba hizi ndizo barabara muhimu za kiuchumi kwahiyo tutazijenga kwa kiwango cha lami na kama kuna barabara nyingine muhimu tunaahidi kuwa tutaanza na kiwango cha changarawe ili ziweze kupitika kwa muda wote." Amesema Dkt. Samia.
Akizungumzia sekta ya nishati Mkoani Kigoma Dkt. Samia pia amesema serikali yake itaendeleza ujenzi wa mradi wa kufua umeme kwenye mto Malagarasi pamoja na ujenzi wa kituo Cha kupooza umeme Kidakwe ili kuondokana na changamoto ya umeme Mkoani humo inayotokana na umbali kutoka unapozalishwa umeme kufika Mkoani humo.
Awali Dkt. Samia pia amesema serikali ya awamu ya sita imefanikisha pia kuokoa zaidi Ya Bilioni 58 zilizokuwa zinatumika kila mwaka kwaajili ya ununuzi wa vipuri na mafuta ya dizeli kwaajili ya majenereta ya umeme baada ya kuiunganisha Kigoma na Gridi ya umeme ya Taifa na hivyo kuondokana na matumizi ya umeme wa majenereta, fedha ambazo zimetumika kusambaza umeme kwenye Vijiji vyote vya Mkoa wa Kigoma.



No comments:
Post a Comment