
Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM, amesema usimamizi mzuri waMfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF, umekuwa na tija kubwa kwa jamii nchini, ikiwezesha kuondoa kundi kubwa la wananchi kwenye lindi la umaskini.
Dkt. Samia katika kuhakikisha wananchi wanaondokana zaidi na umaskini na kupata mahitaji yao muhimu, ameahidi kuwa ikiwa atachaguliwa katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ataendelea pia kusimamia mfuko huo pamoja na kutoa mikopo isiyokuwa na riba ili kuwezesha ukuaji wa biashara ndogo ndogo nchini.
"Ndugu zangu wakati ninafungua kampeni kule Tanzania bara niliahidi kurasimisha biashara ndogo ndogo, hili ni jambo la Muungano na tutakwenda kulifanya pamoja kurasimisha biashara ndogo ndogo bara pamoja na hapa Zanzibar." Ameongeza kusema Dkt. Samia.
Dkt Samia pia katika hotuba yake mbele ya Maelfu ya wananchi na wapigakura wa Zanzibar, amezungumzia mafanikio yaliyopatikana katika serikali ya awamu ya sita, akisema serikali yake imefanikiwa kukuza na kuimarisha uhusiano wa diplomasia pamoja na ulinzi na usalama wa Taifa, akisema heshima inayoipata Tanzania Kimataifa imetokana na umoja na mshikamano unaoshuhudiwa nchini.
Aidha Dkt. Samia amesema mafanikio yote yanayoshuhudiwa na kusemwa kote nchini yametokana na tija ya kuenzi na kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, akihimiza kila Mtanzania kuendelea kuuenzi na kuulinda, akisema Chama Cha Mapinduzi tofauti na wengine kinaamini kuwa Muungano huo umekuwa na manufaa makubwa kwa pande zote mbili ikiwa ndio msingi wa ustawi na maendeleo ya Tanzania, akirejea namna ambavyo Mwalimu Nyerere alivyouita Muungano huo kama Lulu ya Afrika




No comments:
Post a Comment