DKT. SAMIA KUBISHA HODI MKOANI LINDI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, September 24, 2025

DKT. SAMIA KUBISHA HODI MKOANI LINDI



Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Septemba 24, 2025 anatarajiwa kuingia Mkoani Lindi, kuendelea na Kampeni za uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.


Kabla ya kuanza ziara yake kwenye Wilaya za Ruangwa na Mtama Mkoani Lindi, Dkt. Samia atapita Ndanda, Mtwara kwa ratiba yake ya mwisho Mkoani humo, pamoja na mambo mengine akitarajiwa kuzuru Kaburi la Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania na Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi Taifa Hayati Benjamin Mkapa.


Jana Dkt. Samia aliahidi kuongeza maeneo ya ufugaji kutoka ekari Milioni 3.4 hadi kufikia Milioni sita Mkoani Mtwara ili kuondoa changamoto ga migogoro baina ya wakulima na wafugaji, akiahidi pia kuendelea kutoa ruzuku za chanjo kwa wafugaji na wakulima pamoja na kusema wakulima wa mbaazi na ufuta nchini hawatouza mazao yao kwa bei za hasara ikiwa atachaguliwa.


Kuelekea mwaka 2030, kupitia Ilani ya CCM, Dkt. Samia ameahidi kwa Wilaya ya Mtama kujenga daraja la Namupa katika barabara ya Nyangao- Namupa, kufunga taa katika barabara na mitaa mbalimbali, ujenzi wa soko la majengo, ujenzk wa shule mpya 7 za sekondari, pamoja na umaliziaji wa miradi sita ya maji inayotekelezaa kwenye Wilaya hiyo.


Aidha kwa Mtama pia Ilani imeahidi upanuzi wa mradi wa Maji Kitangata- Mtumbikile, Nanjime- Mkwajuni na Nangaru Corridor, uboreshaji mradi wa maji Rondo, kuanzisha mashamba darasa ya mifugo kwenye Kata zote za Mtama, ujenzi wa gridi imara ya umeme ya Kilovoti 220 pamoja na kuanza kutekeleza mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia kuwa kimiminika maarufu kama Liquefied Natural gasi- LNG.


Katika Wilaya ya Ruangwa pamoja na mambo Mengine, CCM imeahidi ujenzi wa maabara 10 na maktaba 10 kwenye shule za sekondari, kuanzisha mashamba ya korosho (block farms) yenye jumla ya ekari 800 katika Vijiji vya Narung'ombe, Namkatila, Mchenga na Mbekenyera, uchimbaji wa visima 5 na usimikaji wa pampu za sola, matenki ya maji na mifumo ya umwagiliaji maji, ujenzi wa majosho 5 kwenye Kata 5, ujenzi wa mabwawa 4 ya samaki pamoja na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha Kimkakati cha uchakataji wa mazao ya Korosho.


Jana Dkt. Samia akiwa Masasi Mtwara alikaririwa akisema huduma za afya, elimu, Maji na umeme kwa Chama Cha Mapinduzi sio miradi ya maendeleo, hivyo shughuli hizo ni wajibu wa Chama Cha Mapinduzi kila wakati katika kukuza na kuimarisha utu wa Mtanzania na kuahidi kasi zaidi katika uendelevu wa kuhakikisha kila Mtanzania anapata stahiki hizo pamoja na mahitaji hayo muhimu kwa kila siku.

No comments:

Post a Comment