Drone za Kizalendo Kutoka Mati Technology Kuleta Mageuzi Kilimo - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 2, 2025

Drone za Kizalendo Kutoka Mati Technology Kuleta Mageuzi Kilimo




Na Mwandishi Wetu.


KAMPUNI ya Mati Super Brands Ltd kupitia tawi lake la Mati Technology imezindua teknolojia mpya ya ndege nyuki (drone) zinazotengenezwa nchini, zenye uwezo wa kuboresha sekta ya kilimo na huduma nyingine za kijamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mati Group of Companies, David Mulokozi, amesema kampuni hiyo imeamua kuwekeza katika uzalishaji wa drone zinazotumika kunyunyizia dawa mashambani, kupima maeneo, kupanda mbegu, kusafirisha mizigo na kusaidia kaguzi mbalimbali.

Mulokozi ameeleza kuwa drone hizo zitauzwa kuanzia Shilingi milioni 17, bei ambayo ni nafuu ukilinganisha na gharama kubwa za kuagiza kutoka nje ya nchi. Pia, kampuni ipo katika mazungumzo na benki ili kuwezesha wakulima kupata mikopo kwa ajili ya kumudu teknolojia hiyo.


“Tumeona changamoto kubwa inayowakabili wakulima hasa kwenye upuliziaji wa dawa. Kwa kutumia drone hizi, hekari moja inaweza kunyunyiziwa dawa ndani ya dakika saba pekee, jambo linaloongeza ufanisi na kulinda afya za wakulima,” alisema Mulokozi.

Aidha, amebainisha kuwa uzalishaji wa drone hizo utatoa ajira kwa wahandisi wa Kitanzania na kufanikisha uhamishaji wa teknolojia kutoka kwa wataalamu wa kigeni

Kwa upande wake, Afisa Ushirika kutoka ofisi ya Msajili mkoa wa Manyara, Godamen Merinyo, amesema teknolojia hiyo ni mkombozi mkubwa kwa wakulima wa mazao kama mbaazi ambayo hukua kwa urefu na kufanya unyunyiziaji wa dawa kuwa mgumu na wa gharama kubwa.

“Hii itasaidia kuongeza uzalishaji kwa gharama nafuu na kuimarisha vyama vya ushirika. Tutaanza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya teknolojia hii,” alisema Merinyo.

Naye Afisa Kilimo wa mkoa wa Manyara, Paulo Eugine, amesema drone hizo zitasaidia kuwalinda wakulima dhidi ya madhara ya kiafya yaliyokuwa yanawapata kutokana na kutumia pampu za mgongoni.

“Sasa mkulima ataweza kutumia remote control bila kuingiliwa na sumu, jambo linaloimarisha usalama na afya zao,” alisisitiza Eugine.


Hatua hii ya Mati Technology inatarajiwa kuchochea mapinduzi ya kilimo nchini na kuunga mkono jitihada za serikali katika kukuza tija kwa kutumia teknolojia za kisasa.

No comments:

Post a Comment