ERB TOENI MOTISHA KWA WAHANDISI: DKT. BITEKO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, September 25, 2025

ERB TOENI MOTISHA KWA WAHANDISI: DKT. BITEKO



Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameitaka Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kuongeza bidii katika kuwapa motisha wahandisi wanaofanya kazi vizuri kwa kuwatambua na kuwapa tuzo ili kuwatia moyo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Ameeleza hayo Septemba 25, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua maadhimisho ya 22 ya Siku ya Wahandisi Tanzania ambayo yamebebwa na kauli mbiu “Wajibu wa Wahandisi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”.

Amesisitiza kuwa uandaaji wa motisha hizo utawafanya wahandisi kuona taaluma yao inathaminiwa na hivyo kuongeza bidii katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Naomba Bodi mfanye kazi nyingine mpya ya kuwapa motisha wahandisi wanaofanya vizuri, fanyeni ufuatiliaji kubaini wale waliosimamia miradi kwa ubora kuliko wengine, tumieni mikutano kama hii au Siku kama ya leo kuwataja na kuwapa zawadi wahandisi, hii itasaidia na wengine kujituma na kushindana zaidi”, amesema Dkt. Biteko

Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono wahandisi wakiwa wanatekeleza majukumu yao kwani taaluma hiyo ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo kwenye nchi kupitia ubunifu wanaoufanya katika miradi mbalimbali.

Aidha, amewataka wahandisi kufanya kazi kwa uaminifu na kwa kuzingatia viapo vya maadili walivyoviapa ili kuipa hadhi na heshima taaluma yao.


Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Wizara ya Ujenzi kupitia ERB itaendelea kuboresha mazingira ya kitaaluma kwa wahandisi pamoja na kuwezesha mafunzo kwa vitendo kupitia mpango wa mafunzo kwa wahandisi wahitimu (SEAP).


Ameongeza kuwa Wizara ya Ujenzi inaendelea kuhakikisha kuwa Wahandisi wazawa wanashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya SGR, bomba la mafuta, miradi ya Barabara na madaraja, viwanja vya ndege, maji na umeme ili kuwaongezea ujuzi.


Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, Wakili, Mhandisi, Menye Manga amesema kuwa mpaka sasa Bodi imesajili wahandisi 44,000, mafundi sanifu 3,445 ambapo amefafanua kuwa idadi hiyo bado haitoshelezi kulingana na mahitaji ya nchi hivyo Bodi inaendelea kushirikiana na Serikali kuhakisha idadi ya wahandisi inaongezeka.


Maadhimisho ya mwaka huu yameshirikisha zaidi ya wahandisi 4,000 kutoka ndani na nje ya nchi ambapo katika maadhimisho hayo Mgeni rasmi alishuhudia kiapo kwa wahandisi wapatao 400 na kuzindua ‘ERB Mhandisi App’ ambayo itasadia wahandisi kuweza kupata taarifa mbalimbali zihusuzo masuala ya kihandisi nchini.






No comments:

Post a Comment