WAFANYABIASHARA WA MADINI WAHIMIZWA KUTUMIA VIPIMO SAHIHI GEITA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, September 25, 2025

WAFANYABIASHARA WA MADINI WAHIMIZWA KUTUMIA VIPIMO SAHIHI GEITA



Afisa Vipimo Mkoa wa Geita Bw. Tumaini Anyitike (katikati) akieleza umuhumu wa kutumia vipimo sahihi katika ufungashaji wa bidhaa kwa wajasiriamali waliotembelea banda la WMA katika maonesho ya Kimataifa ya Teknolojia ya madini Mkoa wa Geita.

.....

Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Geita Bi. Eva Ikula amewataka wafanyabiashara wa madini mkoani humo kuzingatia matumizi ya vipimo sahihi katika biashara yao ili kuhakikisha kunakuwa na usawa kwa pande zote zinazohusika na kuepusha upande wowote kupunjika.

Ametoa wito huo Septemba 25, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya kimataifa ya teknolojia ya madini yanayofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mjini Geita, yenye kaulimbiu “ukuaji wa sekta ya madini ni matokeo ya matumizi ya teknolojia sahihi na uongozi bora, shiriki uchaguzi mkuu oktoba 2025”.

Ikula ameeleza kuwa, WMA ina mchango mkubwa katika sekta ya madini ambapo biashara hiyo haiwezi kufanyika pasipo kuwa na mizani iliyohakikiwa na inayotumika kwa usahihi ili kuhakikisha kunakuwa na usawa baina ya pande mbili zinazofanya biashara.

Kadhalika, amesema kuwa, katika sekta ya madini, mojawapo ya majukumu ya WMA ni kuhakikisha mizani zote zinazotumika kuuzia na kununulia vito na madini zinahakikiwa na zinapima madini kwa usahihi.

Ameongeza kuwa, Wakala pia hutoa ushauri wa kitaalamu kuhusiana na mizani zinazopaswa kutumika kuuzia madini kwa kuwa siyo mizani zote zinastahili kutumika kuuzia na kununulia madini.

“Katika mwaka wa fedha 2025/2026, Mkoa wa Geita unatarajia kuhakiki mizani 197 zinazotumika katika sekta ya madini ambapo mpaka sasa kwa robo ya kwanza, jumla ya mizani 37 zimehakikiwa na kukidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura 340 na zinafaa kutumika katika uuzaji na ununuzi wa madini,” amesema Ikula.

Vilevile, ameeleza kuwa Mkoa wa Geita una jumla ya masoko kumi (10) ya kuuzia na kununulia dhahabu ambayo ni Geita mjini, Katoro, Chato, Lwamgasa, Nyarugusu, Mbogwe, Bukombe, Nyang’wale, Mgusu na Nyakagwe.

Amedadavua kuwa, kutokana na uwepo wa masoko hayo, WMA hufanya kaguzi za kushtukiza mara kwa mara kwa lengo la kujiridhisha kama vipimo vinatumika kwa usahihi ambapo kwa mtumiaji yeyote ambaye hubainika kuchezea vipimo huchukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura 340.

Naye Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa WMA, Bw. Paulus Oluochi amewahimiza wananchi kutembelea banda la WMA katika maonesho hayo ili wapate elimu ya vipimo pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu vipimo mbalimbali.

Oluochi amesema kuwa, inapotokea mtumiaji yeyote wa vipimo akapata changamoto yoyote anapaswa kuwasiliana na ofisi ya WMA iliyopo karibu ili aweze kupata msaada kwa haraka akifafanua kuwa ofisi za WMA zinapatikana katika mikoa yote Tanzania Bara au atoe taarifa kwa namba ya bure ambayo ni 0800 110097.



Katibu Tawala Mkoa wa Geita Bw. Mohamed Gombati (kulia) akikabidhiwa zawadi na Meneja wa WMA Mkoa wa Geita Bi. Eva Ikula mara baada ya kutembelea banda hilo katika maonesho ya Kimataifa ya Teknolojia ya madini Mkoa wa Geita na kupata elimu ya vipimo.



Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Geita Bi. Eva Ikula akitoa ushauri wa kitaalamu kwa mdau katika maonesho ya Kimataifa ya Teknolojia ya madini Mkoa wa Geita.



Afisa Vipimo Mkoa wa Geita Bw. Tumaini Anyitike (katikati) akieleza umuhumu wa kutumia vipimo sahihi katika ufungashaji wa bidhaa kwa wajasiriamali waliotembelea banda la WMA katika maonesho ya Kimataifa ya Teknolojia ya madini Mkoa wa Geita.

No comments:

Post a Comment