FAINALI YA KIHISTORIA SHIMIWI YA 39 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, September 14, 2025

FAINALI YA KIHISTORIA SHIMIWI YA 39


Na Mwandishi Wetu, Mwanza


Fainali za michezo ya 39 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), zitakazofanyika tarehe 16 Septemba 2025 katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, zinatarajiwa kuwa za kihistoria kutokana na uwepo wa timu mpya zilizofuzu kwa michezo ya kuvuta kamba, mpira wa miguu na netiboli.

Miongoni mwa timu zilizovunja rekodi kwa kufika hatua ya fainali kwa mara ya kwanza ni Tume ya Umwagiliaji kwa upande wa mpira wa miguu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi katika netiboli, pamoja na RAS Tanga na TAKUKURU kwa michezo ya kuvuta kamba kwa wanawake na wanaume.

Hata hivyo, pambano hilo linatarajiwa kutoa burudani ya aina yake kutokana na uwepo wa mabingwa watetezi: timu ya Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma katika mpira wa miguu, na timu ya Ofisi ya Rais – Ikulu kwa upande wa netiboli na kamba wanaume.

Katika michezo ya nusu fainali iliyochezwa CCM Kirumba:
Kamba (Wanawake): RAS Tanga waliwavuta Mahakama kwa 2–0, huku TAKUKURU wakiwafunga RAS Geita 2–0.

Kamba (Wanaume): Ikulu waliwazidi Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa 2–0, nao TAKUKURU wakiibuka na ushindi wa 2–0 dhidi ya Wizara ya Uchukuzi.
Mpira wa Miguu: Klabu ya Utumishi waliwafunga TAKUKURU bao 1–0, wakati Tume ya Umwagiliaji waliibuka na ushindi wa bao 1–0 dhidi ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Netiboli: Ikulu waliwazidi Utumishi kwa magoli 53–26, baada ya kuongoza mapumziko kwa 30–16. Nao Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi waliwafunga Wizara ya Maliasili na Utalii kwa magoli 47–42, baada ya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya 22–22.

Mashabiki wa michezo wanatarajia kushuhudia fainali zenye msisimko mkubwa, huku historia mpya ikitarajiwa kuandikwa katika mashindano haya ya mwaka huu.

No comments:

Post a Comment