
Mgombea wa Nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumatatu Septemba 22, 2025 anatarajiwa kuendelea na Kampeni Songea Mjini, Namtumbo na Tunduru Mkoani Ruvuma, akinadi Ilani ya Chama chake pamoja na kuomba kura kwa wananchi.
Jana Jumapili, siku ya kwanza ya kampeni zake Mkoani humo akitokea Visiwani Zanzibar, ambapo pamoja na mambo mengine Dkt. Samia ameahidi kuongeza uzalishaji wa madini kutoka tani 2, 600,000 hadi tani 3,500,000, kutenga maeneo 2 maalum ya wachimbaji wadogo wa madini katika Wilaya za Tunduru na Nyasa pamoja na kuziwezesha halmashauri kunufaika na uchimbaji wa makaa ya mawe.
Ameahidi pia kumalizia uunganishaji wa umeme kwenye Vitongoji vyote vya Mkoa huo, kuanzisha na kukamilisha utekelezaji wa mradi wa uzalishaji wa nishati ikiwemo mradi wa Songea- Mbinga wenye Msongo wa Kilovoti 220, kujenga kituo kidogo cha kupooza umeme Nyasa na kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala.
Dkt. Samia kadhalika ameahidi ujenzi wa skimu 4 za umwagiliaji katika Wilaya za Nyasa, Namtumbo, Songea na Tunduru, kuanzisha vituo 5 vya kukodisha zana za kilimo huko Madaba, Songea Dc, Mbinga Dc, Namtumbo na Tunduru, kuanzisha mashamba 4 makubwa ya kilimo cha pamoja na cha kisasa na kuchimba visima 150 kwa kila Halmashauri kwaajili ya kilimo cha umwagiliaji.
Aliahidi pia kuanzisha na kuendeleza viwanda vya kimkakati ikiwemo kiwanda cha mbolea, sukari, mafuta ya kula na mavazi, kuanzisha viwanda 3 vikubwa vya kubangua Korosho, kukoboa kahawa na kusaga sembe, viwanda vya kati 2 vya kusindika sembe na viwanda vidogo 30 vya kusindika mazao, ufundi, seremala na utengenezaji wa bidhaa za vipodozi pamoja ba kuanzisha kongani 16 za viwanda kwenye maeneo maalumu 16 ya kiuchumi ( SZE's) pamoja na kuanzisha maeneo huru 2 ya biashara.
Kadhalika Dkt. Samia ambaye jana alikuwa ameambatana na Mgombea mwenza wake Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameahidi pia kuimarisha miundombinu ya uvuvi kwa kukarabati na kujenga mialo 3 ya kisasa na masoko 2 ya samaki, kuzalisha vifaranga 100, 000 wa samaki kwaajili ya kufuga kwenye vizimba ziwa Nyasa, kuwezesha upatikanaji wa mitaji/ mikopo kwa wavuvi na wakuzaji wa viumbe maji na kuimarisha mradi wa kituo cha uzalishaji samaki kwa kujenga mabwawa na ukuzaji wa vifaranga katika eneo la Mpitimbi.
No comments:
Post a Comment