
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuthibitisha kuwa ni mama wa maendeleo kwa kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kijamii na kiuchumi nchini.
Akihutubia wananchi wa Jimbo la Kojani, Pemba Jumamosi (Septemba 27, 2025), Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefanikisha ujenzi wa vituo vya afya vyenye uwezo wa kutoa huduma zote za msingi, hali iliyopunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
“Kwa sasa wananchi hawaendi umbali mrefu kupata huduma za afya, wataalamu wa afya wameajiriwa,” alisema.
Alibainisha kuwa Rais Dkt. Samia ametekeleza pia maono yake ya kummtua mama ndoo kichwani kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa, ya kati na midogo ya maji, sambamba na kuvutia wawekezaji waliowekeza katika miradi mikubwa iliyotoa ajira kwa Watanzania.
Majaliwa alisisitiza kuwa Rais Samia ni mgombea pekee mwenye maono ya kuivusha Tanzania, akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Oktoba 29.
Katika mikutano huo, Majaliwa alimpongeza mgombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuifungua Zanzibar kiuchumi na kugusa sekta mbalimbali za kijamii.
“Uongozi wa Dkt. Mwinyi umegusa kila sekta ikiwemo miundombinu, elimu, afya, maji, michezo na huduma nyingine. Ni Daktari wa Maendeleo, nendeni mkamjazie kura,” alisema.
Aidha, Majaliwa alimnadi Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kojani, Hamad Chande, akimtaja kuwa ni mtendaji, mzalendo na mchapa kazi.
“Ninamfahamu Chande. Ndiyo maana aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha. Mchagueni ili aendelee kuwaletea maendeleo,” alisema.
Kwa upande wake, Chande aliwaomba wananchi wa Jimbo hilo kumpa ridhaa ya kuendelea kuwa mbunge wao, akiahidi kusimamia kikamilifu shughuli za maendeleo.




No comments:
Post a Comment