
Na Mwandishi Wetu , Dodoma
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amewataka waandishi wa habari kuzingatia maadili na uhalisia katika kuripoti habari za uchaguzi ili kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi.
Akifungua mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu Uchaguzi na Usalama yaliyofanyika Septemba 27, 2025 jijini Dodoma, chini ya uratibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma (DPC), Waziri Mavunde alisema tasnia ya habari ni mhimili muhimu kuelekea uchaguzi.
“Waandishi wa habari ni nguzo kubwa ya jamii. Habari isiyo sahihi inaweza hata kuvuruga amani. Niwaombe tusimame katika taaluma yetu, tufuate maadili na tufanye kazi kwa usawa bila upendeleo,” alisema.
Amesisitiza kuwa wananchi wanategemea kupata taarifa sahihi ili waweze kufanya maamuzi ya busara.
“Mara nyingine mwandishi anamwandika mgombea amepokewa na mafuriko ya watu, lakini picha zinaonesha hawazidi hamsini. Hii haijengi heshima. Tuhabarishe kwa uhalisia, tuwasaidie wananchi kufanya maamuzi sahihi,” aliongeza.
Aidha, Waziri Mavunde aliwahimiza wanahabari kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi kwa kutumia haki yao ya kikatiba.
“Watanzania lazima washiriki uchaguzi. Ninyi wanahabari mna jukumu la kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kupiga kura na kuwachagua viongozi watakaoongoza kwa miaka mitano ijayo,” alisema.
Waziri Mavunde pia alisisitiza wajibu wa waandishi wa habari wa Mkoa wa Dodoma kutoa taarifa sahihi kuhusu changamoto za wananchi na ahadi za wagombea.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa DPC, Katare Mbashiru, alisema mafunzo hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kujifunza mbinu bora za kuripoti uchaguzi kwa weledi na kuzingatia maadili ya taaluma.
“Mafunzo haya yameongeza uelewa kuhusu sheria, kanuni na matumizi ya teknolojia katika upashanaji habari. Yataleta tija kwa waandishi wa Dodoma kuhakikisha wanabaki kuwa waandishi wa kuaminika na walinzi wa demokrasia,” alisema.






No comments:
Post a Comment