
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mgombea Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Mtumba, Ndg. Anthony Mavunde, ameendelea na kampeni zake kwa kishindo ambapo Septemba 26, 2025 alihutubia wananchi wa Kata ya Ngh’ongh’ona na kutoa ahadi mbalimbali za maendeleo kwa jimbo hilo.
Katika mkutano huo wa hadhara, Mavunde aliwashukuru wananchi kwa mshikamano wao na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mageuzi makubwa yanayoendelea nchini katika sekta za afya, elimu, maji, barabara na nishati.
Miongoni mwa miradi aliyobainisha ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya Ngh’ongh’ona, ukamilishaji na usajili wa Shule ya Sekondari Mapinduzi, pamoja na upimaji na umilikishwaji wa ardhi kwa wananchi. Pia aliahidi kuchimba visima vipya vya maji safi katika maeneo ya Mhande na Kwa Mjeni, pamoja na kuongeza kina cha bwawa la umwagiliaji.

Aidha, Mavunde alisema kuwa kipaumbele chake kitakuwa kusimamia ujenzi wa soko na stendi ya mabasi, ukamilishaji wa usambazaji wa nishati ya umeme katika maeneo yote yaliyosalia, na ununuzi wa mtambo wa kisasa wa kufungua barabara (Motor Grader) kwa ajili ya jimbo hilo.
Vilevile, aliahidi kuanzisha viwanda vidogo kupitia mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, pamoja na kuanzisha klabu za wazee kata mbalimbali. Katika sekta ya elimu, alibainisha mpango wa ununuzi wa mashine kubwa za kudurufu mitihani kwa kila kata.
Mavunde pia aliahidi kushughulikia mgogoro wa ardhi maeneo ya Itumbi na Mapinduzi B, ukamilishaji wa Zahanati ya Mapinduzi B, na ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara ya Ntyuka–Mvumi–Kikombo.
Kwenye sekta ya michezo, alitangaza kuanzishwa kwa mashindano maalum ya mpira wa miguu maarufu kama “Mavunde Cup” yatakayoshirikisha kata zote za jimbo hilo.
Aidha, aliahidi kuanzisha ujenzi wa vivuko vya watembea kwa miguu na magari pamoja na ukarabati mkubwa wa barabara ya Ngh’ongh’ona–Mapinduzi–Chololo.
Wananchi walioshiriki mkutano huo walimpongeza kwa kuwa karibu na jamii na kutoa ahadi zinazogusa maisha yao ya kila siku, huku wakiahidi kumpa kura za kishindo ifikapo siku ya uchaguzi.





No comments:
Post a Comment