NAMIBIA WACHANGAMKIA KISWAHILI, WAZIRI GWAJIMA AKIPONGEZA CHUO CHA TRIUMPHANT - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, September 8, 2025

NAMIBIA WACHANGAMKIA KISWAHILI, WAZIRI GWAJIMA AKIPONGEZA CHUO CHA TRIUMPHANT



Na WMJJWM - Windhoek, Namibia


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima , amekipongeza Chuo cha Triumphant cha nchini Namibia kwa juhudi za kufundisha lugha ya Kiswahili nchini humo.

Dkt. Gwajima ametoa pongezi hizo Septemba 5, 2025 alipotembelea chuo hicho kilichoanzishwa na kumilikiwa na Mtanzania, Profesa Geoffrey Kiangi, tangu mwaka 2006.

“Kiswahili siyo tu lugha bali ni chombo cha historia yetu, tamaduni zetu na umoja wetu wa kikanda. Nakipongeza Chuo cha Triumphant kwa kusimama kama mfano mzuri wa jinsi elimu na tamaduni zinavyoweza kuwa msingi wa urafiki wetu katika kujenga Afrika tunayojifunza pamoja, tunakua pamoja na tunashinda pamoja,” alisema Dkt. Gwajima.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Ceasar Waitara, ameeleza namna Ubalozi unavyoratibu ushirikiano wa Tanzania na Namibia katika nyanja mbalimbali, ikiwemo kukuza lugha ya Kiswahili. Amebainisha kuwa tayari BAKITA imeingia makubaliano na Chuo hicho na mwalimu kutoka Tanzania anatarajiwa kuanza kufundisha Kiswahili kwa viongozi wa Namibia kuanzia Oktoba, 2025.

Naye Mkuu wa Chuo cha Triumphant, Prof. Geoffrey Kiangi, amesema chuo chake kinajivunia historia ya uhusiano wa Tanzania na Namibia kwa kuanzisha programu za kitaaluma zinazoshirikisha mataifa hayo.

Amempongeza pia Balozi Waitara kwa mchango wake katika kukuza urafiki huo. Wanafunzi wa Kiswahili wa chuo hicho walionesha umahiri wao kwa kutoa salamu na kuimba nyimbo kwa Kiswahili, huku Waziri Gwajima na msafara wake wakijumuika nao.

Chuo hicho kilianzisha kozi ya Lugha ya Kiswahili kwa wanafunzi wapatao 80 wanaofundishwa kupitia mtandao kwa ushirikiano na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA). Aidha, chuo hicho kina ushirikiano na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Kwa sasa, Kiswahili kinazungumzwa na watu wapatao milioni 200 barani Afrika na kimetambuliwa kama lugha ya kikazi katika Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Katika ziara hiyo, Waziri Dkt. Gwajima ameambatana na mjane wa Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa, mama Anna Mkapa, baada ya ratiba ya Mkutano Mkuu wa Wajane Barani Afrika uliofanyika Septemba 3–5, 2025 jijini Windhoek, Namibia ambapo Dkt. Gwajima alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.







No comments:

Post a Comment