
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imezitaka taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi na weledi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndugu. Kailima Ramadhani leo tarehe 08 Septemba, 2025 wakati akifungua kikao kazi cha Tume na taasisi na asasi hizo kilichofanyika Mkoani Dodoma.
”Ni vyema mkafahamu kuwa kifungu cha 10(1)(g) na (h) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024 na kanuni ya 22 na 23 ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024, zimeipa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi mamlaka ya kutoa elimu ya mpiga kura nchini, kuratibu na kusimamia taasisi na asasi zinazotoa elimu hiyo.

Hivyo, kazi mnayoenda kuifanya ni moja ya majukumu ya kisheria ya Tume na mnapaswa kuifanya kwa weledi na ufanisi mkubwa,” amesema.
Ndugu Kailima ameongeza kuwa, Tume inatarajia kuona kuwa, taasisi na asasi za kiraia zinatoa elimu iliyolengwa haswa kwa kutoa kipaumbele kwenye mambo ambayo yatawapa wananchi, wagombea na vyama vya siasa kwa ujumla uelewa wa namna ya kushiriki kwenye kampeni kwa amani na utulivu ikiwa ni pamoja na kupata uelewa mzuri wa utaratibu wa kupiga kura.
”Hatutarajii kabisa mtoe elimu ambayo italeta mkanganyiko kwenye jamii na kuiingiza nchi kwenye machafuko kama ilivyotokea katika maeneo mengine hapa Afrika na duniani kwa ujumla,” amesema.
Amesisitiza kuwa taasisi na asasi hizo haziruhusiwi kuwapa watu wengine au taaisi au asasi nyingine vibali walivyopewa na kwamba vibali hivyo ni lazima vitumiwe na walengwa tu.
”Nyie ndio mabalozi wa Tume, hivyo, mhakikishe katika kipindi chote cha utekelezaji wa jukumu lenu la kutoa elimu, mnazingatia Katiba, sheria, kanuni na maelekezo ambayo Tume imekuwa ikiyatoa mara kwa mara,” amesema.
Kikao kazi hicho kiliwaleta pamoja viongozi wa Tume na wawakilishi wa taasisi na asasi 164 zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa.

No comments:
Post a Comment