Na Mwandishi Wetu - MOROGORO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, amewataka watendaji wa Tume ya Madini nchini kuendelea kuimarisha usimamizi wa Sekta ya Madini kupitia usimamizi madhubuti wa leseni za madini, utatuzi wa migogoro kwenye uchimbaji wa madini pamoja na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za mnyororo wa thamani wa madini ili sekta hiyo iendelee kutoa mchango mkubwa katika Pato la Taifa.
Akizungumza katika kikao cha Menejimenti ya Tume ya Madini kilichofanyika mkoani Morogoro, Mhandisi Samamba amesisitiza umuhimu wa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha leseni zinazotolewa kwa wachimbaji zinaendelezwa kwa mujibu wa masharti ya leseni hizo, akibainisha kuwa Serikali haitasita kufuta leseni zisizoendelezwa na kuzipatia kwa wawekezaji au waombaji wenye uwezo na dhamira ya kuziendeleza.
Aidha, amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kushughulikia migogoro inayojitokeza katika shughuli za uchimbaji kwa wakati na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo, badala ya kusubiri wahusika kufikisha migogoro hiyo katika ngazi za juu za maamuzi.
Katika kikao hicho kilichoshirikisha pia viongozi mbalimbali wa taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini, Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo, Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa Mhandisi Samamba ameipongeza Tume ya Madini kwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli.
Amesema kuwa kuanzia Julai 2025 hadi sasa, Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya shilingi trilioni 1.36, sawa na asilimia 113.34 ya lengo la mwaka wa fedha 2025/2026, na kuwataka watendaji kuendelea kubuni mikakati mipya itakayowezesha Tume kuvuka lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.4 katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Katibu Mkuu pia ameelekeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuweka kipaumbele katika usimamizi wa afya, usalama na mazingira kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini, hususan kwa kutoa elimu endelevu kwa wachimbaji wadogo wa madini na kuimarisha ukaguzi katika maeneo ya shughuli za uchimbaji.
Akizungumzia jitihada za Serikali za kudhibiti utoroshaji wa madini, Mhandisi Samamba amesema mikakati iliyowekwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi katika mnyororo mzima wa thamani wa madini kuanzia uzalishaji hadi usafirishaji, kuendelea kuanzisha masoko na vituo vya ununuzi wa madini, kuweka bei elekezi zinazoendana na soko la dunia pamoja na kuondoa baadhi ya vikwazo vya tozo na kodi vinavyoathiri biashara ya madini.
“Kwa kushirikiana na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, Tume ya Madini imeendelea kutoa elimu ya uzalendo kwa wadau wa sekta ili wawe mabalozi wazuri wa rasilimali za taifa, hasa ikizingatiwa kuwa wachimbaji wadogo wa madini wanachangia takribani asilimia 40 ya mapato yatokanayo na sekta ya madini,” amesema Mhandisi Samamba.
Aidha, amesema Serikali imeidhinisha kutengwa kwa asilimia 10 ya mapato yanayotokana na Sekta ya Madini kwa ajili ya kugharamia tafiti za kina za madini, hatua inayotarajiwa kuongeza ugunduzi wa rasilimali mpya na kuchochea uwekezaji katika sekta hiyo.
Akihitimisha hotuba yake, Mhandisi Samamba amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuendelea kusimamia sekta hiyo kwa uzalendo, uwajibikaji na ubunifu kupitia watumishi waliopo chini yao ili kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo na rasilimali za madini.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, amempongeza Mhandisi Samamba kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na mshikamano kati ya taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini, hatua ambayo imechangia utulivu na maendeleo ya Sekta ya Madini nchini.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, ameishukuru Wizara ya Madini kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kupitia upatikanaji wa vifaa mbalimbali, ikiwemo magari na mashine za kupima madini ya metali, huku akisisitiza kuwa Tume itaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa lengo la kufikia matarajio ya wananchi na taifa kwa ujumla.










No comments:
Post a Comment