SENYAMULE AZITAKA HALMASHAURI DODOMA KWENDA KASI SAWA NA WAWEKEZAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 24, 2026

SENYAMULE AZITAKA HALMASHAURI DODOMA KWENDA KASI SAWA NA WAWEKEZAJI



Na Okuly Julius, OKULY BLOG - DODOMA


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amezitaka Halmashauri zote za Mkoa huo kufanya kazi kwa kasi na ufanisi ili kuendana na kasi ya wawekezaji wa sekta binafsi, akisisitiza kuwa ucheleweshaji wa huduma unaweza kudhoofisha maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Senyamule ametoa kauli hiyo Juni 24, 2026 jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa ofisi za kampuni ya Landmax Real Estate Company Limited.

Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga sekta binafsi kuchangia asilimia 70 ya Pato la Taifa, hivyo taasisi za umma zinapaswa kuhakikisha zinatoa huduma kwa wakati ili kuwezesha wawekezaji kutekeleza shughuli zao bila vikwazo.

“Ukiichelewesha sekta binafsi, unakuwa unadhoofisha mchango wao katika ujenzi wa Taifa. Ni muhimu Halmashauri na taasisi nyingine za umma kufanya kazi kwa kasi inayolingana na wawekezaji,” amesema Senyamule.

Aidha, amesema uwekezaji unaofanyika Dodoma unaendelea kuufanya mji huo kukua kwa kasi na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi.

Akizungumzia sekta ya ardhi, Senyamule amesema thamani ya ardhi katika Mkoa wa Dodoma imeongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali pamoja na sekta binafsi.

“Kwetu sisi ardhi ya Dodoma ni utajiri. Ndiyo maana tunasema dhahabu ya Dodoma ni ardhi. Ukuaji wa thamani ya ardhi hapa ni mkubwa sana,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Landmax Real Estate Company Limited ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbozi, Onesmo Mnkondya, amesema kampuni hiyo imeanzishwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi kupata ardhi salama na makazi bora huku ikichangia kupunguza migogoro ya ardhi.

Aidha, amebainisha kuwa Landmax inatoa huduma mbalimbali ikiwemo uuzaji na ununuzi wa ardhi na mali isiyohamishika, ushauri wa uwekezaji wa ardhi, usimamizi wa mali, urasimishaji wa nyaraka za ardhi, uendelezaji wa miradi, tafiti za soko pamoja na ushirikiano katika miradi ya maendeleo.

Amewataka wananchi na madalali wanaohusika na biashara za ardhi kutumia huduma za kampuni hiyo ili kufanya uwekezeja kwa usalama na kuondokana na migogoro inayotokana na mauzo au ununuzi usio rasmi wa ardhi.

“Tunawaalika wananchi na madalali wote wanaotaka kununua au kuuza ardhi kufika ofisini kwetu ili wapate huduma bora na salama,” amesema Mnkondya.

Naye Balozi wa Landmax na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Clayton Chipando maarufu Baba Levo, amesema kampuni hiyo imekuja kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za utapeli wa ardhi ambazo zimekuwa zikiwakumba wananchi wengi katika Mkoa wa Dodoma.

Amesema kupitia huduma za kitaalamu zinazotolewa na Landmax, wananchi watapata uhakika wa umiliki wa ardhi na kufanya uwekezaji wao kwa kujiamini zaidi.

Amesema kuwa wananchi wanaweza kutumia kampuni hiyo kupata huduma mbalimbali ikiwemo kununua, kuuza na kupangisha nyumba au viwanja kwa kuzingatia taratibu sahihi za kisheria.

Aidha, amewataka madalali wa ardhi kushirikiana na kampuni hiyo ili kuhakikisha miamala yote inafanyika kwa uwazi na usalama, huku nyaraka zote zikihakikiwa ili kuondoa migogoro na vitendo vya utapeli.












No comments:

Post a Comment