
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) utakuwa chachu ya kukuza ujuzi wa wataalamu wa afya nchini.
Prof. Nombo ametoa kauli hiyo Septemba 22, 2025 Jijini Dar es Salaam akifungua kikao cha kwanza cha Kamati ya Uendeshaji ya mradi huo, kilichofanyika katika Kituo cha Umahiri kilichopo Mloganzila, ambapo ameeleza kuwa mradi huo ni kielelezo tosha namna Serikali inavyowekeza katika kuimarisha elimu ya afya na kuhakikisha taifa linapata wataalamu mahiri wa kutoa huduma bora kwa wananchi.
“MUHAS inatoa utaalamu wa kisayansi na kuandaa wataalamu wa afya mahiri. Kituo hiki ni mahali pa kufundisha mabingwa na bobezi katika sayansi ya moyo na mishipa ya damu. Tunaona kina vifaa vya kisasa, hivyo wananchi watanufaika na huduma bora zitakazotolewa hapa,” amesema Prof. Nombo.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu kilichopo Mloganzila, pamoja na ushirikiano wa kimataifa uliowezesha chuo hicho kupata ufadhili wa vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia.
Prof. Kamuhabwa amesema kuwa mchango wa Serikali na wadau wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali umeimarisha uwezo wa MUHAS katika kutoa mafunzo ya kibingwa na kuendeleza tafiti za kisayansi.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa kitaalamu wa MUHAS katika kutoa mafunzo ya vitendo na huduma za kibingwa, sambamba na kuimarisha miundombinu ya kisasa kwa ajili ya tafiti na mafunzo ya afya ya moyo na mishipa ya damu.






No comments:
Post a Comment