TARURA KUSHIRIKIANA NA KAMPUNI YA SUKARI KILOMBERO KUFANYA MATENGENEZO YA BARABARA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, September 22, 2025

TARURA KUSHIRIKIANA NA KAMPUNI YA SUKARI KILOMBERO KUFANYA MATENGENEZO YA BARABARA.




Kilombero-Morogoro


Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Sukari ya Kilombero (KSC) wamekubaliana kuanzisha Mfuko wa Barabara kwa ajili ya matengenezo ya barabara kuu za usafirishaji ndani ya wilaya za Kilosa na Kilombero mkoani Morogoro zenye urefu wa Km 206.

Utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2025/26 ambapo fedha hizo zitatumika kulipia huduma za matengenezo na ukarabati wa barabara za umma zilizo nje ya mashamba ya Kilombero kwa ajili ya kusafirisha miwa kwenda viwandani K1, K2 na K4.

Kamati ya Mfuko wa Barabara imeweka kipaumbele kwa kazi za awali za matengenezo kwenye barabara zilizotengwa za usafirishaji ndani ya wilaya za Kilosa na Kilombero ambapo barabara zilizotambuliwa kwa ajili ya matengenezo ni sehemu ya mtandao mkuu wa barabara za usafirishaji na zinajumuisha barabara zinazosimamiwa na TARURA.

Jumla ya Kilomita 206 za barabara zitafanyiwa matengenezo, ikiwa kilomita 124.90 ni kwa barabara za wilaya ya Kilombero na kilomita 81.70 kwa barabara za wilaya ya Kilosa.

Lengo kuu la mpango huo ni kuziboresha barabara hizo kwani hatua hiyo ni muhimu ili kuhakikisha usafirishaji wa miwa hadi viwandani na pia kusaidia jamii zinazozunguka maeneo hayo.

Mkandarasi atakayehusika na utekelezaji wa kazi hizo ni UNITRANS Tanzania Ltd.

No comments:

Post a Comment