
Akionesha kutambua na kuheshimu kazi yao: jukumu analolijua vyema tamu na chungu zake naye aliposhiriki akiwa Muongoza Watalii katika filamu ya “Tanzania: The Royal Tour,” Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewapongeza na kuwataka waendeleze kazi hiyo kwa ubunifu zaidi.
Rais Samia ametoa salam hizo usiku wa Septemba 27, 2025 kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi aliyekuwa Mgeni Rasmi katika Usiku wa Tuzo za 10 za Waongoza Watalii zijulikanazo kama “Safari Field Challenge” zinazodhaminiwa na kuoneshwa kila mwaka kupitia Azam TV zilizofanyika mjini Karatu, Arusha.
“Mhe Rais anafahamu leo ndio fainali za Tuzo hizi na katika Siku hii pia ya Utalii Duniani amesema niwafikishie salaam za upendo waongoza watalii wenzake kote nchini lakini pia ameahidi kwa ujumla wake kuendelea kuiimarisha sekta ya utalii,” alisema Dkt. Abbasi.
Katika fainali hizo, Rais pia amewashika mkono waongoza watalii wote 10 walioingia fainali kwa kuwapatia fedha za kujikimu watakaporejea katika majukumu yao.
“Amesema kwa kuwa naye ni muongoza watalii mwenzenu naye anaongezea pale wadhamini wengine walipotoa na ametoa milioni 2 taslimu kwa kila mshiriki na milioni tatu tatu taslimu kwa wale washindi wawili,” alisema Dkt. Abbasi akikabidhi fedha hizo kwa niaba ya Rais.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Mshindi wa Tuzo ya Mwongoza Watalii Bora wa Mwaka kwa upande wa wanawake Neema Amosi Singita amemshukuru Rais Samia kwa “sapraizi” ya zawadi.
“Sikutegemea zawadi hizi kutoka kwa Rais. Tunamshukuru sana na tunamuahidi kuwa sisi waongoza watalii wa kike hatutamuangusha,” alisema




No comments:
Post a Comment