SHAMBA LA MITI SILAYO LILIVYOWAKOMBOA WANANCHI WA CHATO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 30, 2025

SHAMBA LA MITI SILAYO LILIVYOWAKOMBOA WANANCHI WA CHATO


Wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Shamba la Miti Silayo, wilayani Chato, mkoani Geita, wameipongeza na kuishukuru Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuwashirikisha moja kwa moja kunufaika na uwepo wa shamba hilo.

Wakizungumza na waandishi wa habari, wananchi hao walisema miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Shule ya Msingi Silayo, miradi ya maji, zahanati, utoaji wa ajira, shughuli za ufugaji nyuki, kuruhusiwa kufanya kilimo pamoja na kugawiwa miche ya miti bure.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Butengo, Kija Mahinza, alisema hapo awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata maji safi na huduma za afya, lakini sasa huduma hizo zinapatikana jirani na maeneo yao.

“Tulikuwa tunapata tabu kubwa ya maji na hata huduma za afya. Kwa sasa tunatibiwa karibu na makazi yetu, jambo ambalo limeleta nafuu kubwa kwa wananchi,” alisema Mahinza.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mikonto, Rupili Stefano Maganyiro, alisema TFS imeleta maendeleo ya kweli kwa vijiji hivyo kupitia miradi ya kijamii na ajira zinazotolewa kwa wakazi wa eneo hilo.

Mkazi wa Butengo, Prisca Jacko, alieleza kuwa wanufaika wakubwa wa uwepo wa shamba hilo ni wanawake na vijana ambao sasa wamepata fursa za kujiajiri kupitia kilimo na ufugaji nyuki.

Naye mkazi wa Butengorumasa, Joseph Ruhazi Kayanda, alisema ugawaji wa miche ya miti bure umewasaidia wananchi kupanda miti katika mashamba yao na kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Msingi Silayo, Mwalimu Gilbert Kayena, aliishukuru TFS kwa kujenga shule hiyo na kusema imesaidia kupunguza tatizo la watoto kutembea umbali mrefu kufuata elimu.

“Shule hii imekuwa mkombozi mkubwa kwa watoto wetu. Kabla ya kujengwa, wanafunzi walilazimika kutembea zaidi ya kilometa tano kufuata shule,” alisema Kayena.

Mhifadhi Mwandamizi wa Shamba la Miti Silayo, Juma Mwita Mseti, alisema TFS imeanzisha miradi mingi ya kijamii na kugawa miche ya miti kwa wananchi ili kuunga mkono juhudi za kuhifadhi mazingira.

“Tumejipanga kuhakikisha jamii inashirikiana nasi kulinda mazingira. Kupitia miche tunayogawa bure, tunahamasisha wananchi kupanda miti na kuepuka uharibifu wa misitu,” alisema Mseti.

Aliongeza kuwa uwepo wa Shamba la Miti Silayo umekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi na mazingira, huku akiwahimiza kuendelea kujenga tabia ya kulinda misitu na kuendeleza shughuli za maendeleo zinazozingatia uhifadhi.

Shamba la Miti Silayo lilianzishwa kwa lengo la kurejesha hali ya mazingira katika hifadhi ya Kahama-Biharamulo, ambayo iliharibiwa na shughuli za kibinadamu ikiwemo ukataji miti, ufugaji wa kuhamahama, uchomaji mkaa na kuni pamoja na makazi ya kudumu ndani ya hifadhi hiyo.


No comments:

Post a Comment