
Shirika la Kutetea Haki za Abiria Tanzania (SHIKUHA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi limefanya kikao maalum na viongozi wa vyama vya daladala jijini Arusha, kikiwa na lengo la kuimarisha huduma kwa abiria na kusisitiza nidhamu miongoni mwa madereva na makondakta.
Kikao hicho kilichofanyika katika stand ndogo ya Arusha kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Taifa wa SHIKUHA, Solomon Nkiggi, Naibu Mkurugenzi wa Elimu na Operesheni, Godwin Mpinga pamoja na Mlinzi wa Usalama wa Abiria, Koplo Alfredy Mtawali.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Nkiggi alisema utoaji wa tiketi ni haki ya msingi ya kila abiria na ni njia ya kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika sekta ya usafirishaji. Alibainisha kuwa tiketi si kielelezo cha malipo pekee, bali pia ni nyaraka muhimu katika kudai fidia au kuwasilisha malalamiko endapo changamoto zitajitokeza safarini.
SHIKUHA pia imesisitiza umuhimu wa madereva na makondakta kuvaa sare rasmi na kuwa nadhifu wakati wa kazi. Hatua hiyo inalenga kuongeza heshima ya taaluma ya usafirishaji, kuimarisha nidhamu, na kuondoa usumbufu kwa abiria kwa kuwawezesha kutambua kwa urahisi wahusika wa vyombo vya usafiri.
Kwa upande wake, Koplo Mtawali aliwataka watoa huduma kuhakikisha usalama wa abiria na mizigo yao muda wote wanapokuwa safarini, akisisitiza kuwa ulinzi wa mali za abiria ni sehemu ya huduma bora.
Viongozi wa vyama vya daladala mkoani Arusha wamelipokea agizo hilo kwa mikono miwili na kuahidi kushirikiana na SHIKUHA pamoja na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha abiria wanapata huduma kwa weledi na kwa kufuata sheria na taratibu.
SHIKUHA imesisitiza kuwa mikutano na mafunzo ya aina hii itaendelea kufanyika mara kwa mara, kwa lengo la kulinda haki za abiria, kuongeza nidhamu katika sekta ya usafirishaji na kutatua changamoto kupitia mazungumzo na mshikamano.

No comments:
Post a Comment