Michezo ya makundi ya SHIMIWI ilikuwa migumu - Washiriki - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 5, 2025

Michezo ya makundi ya SHIMIWI ilikuwa migumu - Washiriki



Na Mwandishi Wetu, Mwanza


Washiriki wa michezo ya 39 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), inayoendelea jijini Mwanza wamesema hatua ya makundi imekuwa ngumu kutokana na kila timu inataka kusonga hatua ya 16 bora.

Mchezaji wa kuvuta kamba Bw. Hija Adam wa Hazina SC amesema michezo ilikuwa ni migumu na hayakuwa marahisi, kwani watu walidhani kwenye makundi wanaweza kupata timu vibonde na kuwavuta kirahisi.

“Watu walidhani mashindano yatakuwa mepesi kwa kweli yalikuwa magumu sana hakukuwa na timu yenye kutoa pointi kirahisi karibu zote zilikuwa ngumu na zenye kuleta ushindani mkubwa, tunashukuru tumeweza kuvuka kwa hatua ya 16 bora na tunakipindi cha kurekebisha makosa ya nyuma,” amesema Bw. Adam.

Naye Bw. Bryson Amon wa timu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), amesema mashindano yalikuwa mazuri na lengo lake limetimia kwa kuwaweka watumishi kuwa vyema kiakili na kimwili, na ametoa wito kwa ambao hawajashiriki waweze kushiriki kwa mwakani.

Nahodha wa Hazina SC, Halima Juma amesema kwa ujumla michezo ya 39 ya SHIMIWI imeendeshwa vizuri, na hata hali ya viwanja na mazingira yote sio mabaya.

Ametoa wito kwa waandaaji kuhakiki kanuni na taratibu za ushiriki wa michezo hii zinafuatwa kwa wachezaji ambao hawana vigezo vya kushiriki kwenye michezo hii, wasiruhusiwe kushiriki.

Kwa upande wake mchezaji Joseph Mroki kutoka timu ya Ofisi ya taifa ya Mashtaka amesema michezo hii imejenga mahusiano mazuri na watumishi wenzao, ambapo pia kumekuwa na ushindani kwa kiasi fulani.

Bw. Joseph ametoa wito kwa timu zinazochukua wachezaji wasio watumishi wa umma maarufu kama mamluki, wahakikishe wanawatumia watumishi halali ili kutimiza lengo la mashindano, ambalo ni kujenga afya na mahusiano, na sio kutafuta ushindi kwa lazima.

Mchezaji Enzania Eshabakhi wa RAS Kagera, amesema mashindano yamekuwa mazuri pamoja na changamoto kadhaa ikiwemo ya upande wa kamba waangalie hatua za makundi kwa kuchanganya timu kutoka kwenye wizara na zile za Ofisi za Wakuu wa Mikoa (RAS).

Kwa upande wake Bw. Herman Lukindo wa UCSAF amesema michezo hii ni mizuri inakutanisha watu mbalimbali na inasaidia kuuweka mwili sawa na inajenga afya na kisaikolojia, hivyo ameipongeza serikali ya awamu ya Sita ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu michezo hii.

Keptaini wa timu ya netiboli ya Wizara ya Nishati, Juliana Peter amesema wameweza kuongeza ujuzi kwenye michezo kwa kupangiwa na timu kutoka RAS, ila ametoa wito kwa waandaaji wa michezo, kuhakikisha timu zinachanganyika. Nishati imevuka inasubiri kucheza hatua ya 16 bora.

Katibu wa RAS Shinyanga, Deus Pascal amesema mashindano yalikuwa mazuri kwa hatua ya makundi, lakini hatua ziboreshwe kwa upande wa waamuzi kwa kuwa na weledi zaidi.

Wakati huo huo, matokeo ya michezo ya kuvutana kwa kamba kwa wanawake timu ya Wizara ya Uchukuzi waliwavuta Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa 1-0; huku Wizara ya Ardhi wametoshana nguvu na Wizara ya Madini kwa 1-1; nayo Tume Sheria walitoka sare na Ofisi ya Bunge kwa 1-1; na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji waliwashinda Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa 2-0; wakati RAS Geita waliwashinda Wizara ya Maji kwa 2-0 na Wizara ya Maliasili na Utalii waliwavuta Wizara ya Mawasiliano kwa 2-0.

Katika michezo ya mpira wa miguu iliyofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana, timu ya Wizara ya Ujenzi waliwachapa wenyeji RAS Mwanza magoli 5-1; huku TAKUKURU wakiwaliza Waziri Mkuu Kazi kwa 9-0 na Wizara ya Mifugo wakishinda RAS Dodoma kwa 4-0; wakati michezo iliyochezwa shule ya sekondari ya wavulana ya Bwiru, timu ya Maendeleo ya jamii waliwashinda Bunge kwa 1-0; huku Katiba na Sheria wakitoka suluhu na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Michezo mingine iliyofanyika uwanja wa Sabasaba timu ya mahakama waliwashinda Wizara ya Madini kwa 2-1; nazo Wizara ya Kilimo walitoka suluhu na OSHA; huku mechi iliyofanyika uwanja wa Mabatini timu ya Ofisi ya Rais Uwekezaji walifungwa na Tume ya Umwagiliaji kwa magoli 4-1; nayo Wizara ya Uchukuzi waliwashinda RAS Kilimanjaro kwa 4-0.






No comments:

Post a Comment