TAKUKURU MWANGA YAFANIKISHA TSH. 24.1 MIL YA MATIBABU KUREJESHWA SERIKALINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, September 20, 2025

TAKUKURU MWANGA YAFANIKISHA TSH. 24.1 MIL YA MATIBABU KUREJESHWA SERIKALINI



Fedha hizo zimerejeshwa baada ya TAKUKURU (W) MWANGA kushinda shauri la jinai namba 25889/2024 dhidi ya mshtakiwa Bi. HADIJA ATHUMANI RAMADHANI ambaye ni Mwalimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ambaye alikuwa anatuhumiwa kwa makosa matatu ambayo ni; Kughushi chini ya vifungu vya 333,335(a) na 337 vya Sheria ya Kanuni za Adhabu Marejeo ya Mwaka 2002, Kuwasilisha nyaraka zenye maelezo ya uongo chini ya kifungu cha 342 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu Marejeo ya Mwaka 2002 na Kuisababishia mamlaka hasara (Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya - NHIF) kiasi cha Tshs. 48,364,040/=) chini ya jedwali na 10 pamoja na vifungu vya 57 na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Marejeo ya Mwaka 2002.

Mtuhumiwa alifanya udanganyifu kwa kutengeneza cheti cha ndoa ili kumuongeza mtegemezi ambaye alidai kuwa ni mume wake na kukiwasilisha kwa mwajiri wake na kupelekea mtu huyo aliyemuongeza kama mwenza wake kupata matibabu kinyume na utaratibu.

Mshitakiwa Bi. Hadija ametiwa hatiani baada ya kuomba kufanya makubaliano (Plea Bargain) kwa nia ya kukiri makosa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Wakili wa Serikali Bi.FURAHINI KIBANGA mbele ya Mhe. BARAKA KABURURU - Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Mwanga aliieleza Mahakama kuwa mshitakiwa aliandika barua kwa DPP kuomba kukiri makosa na kumaliza shauri kwa njia ya makubaliano.

Baada ya makubaliano kumalizika mkataba wa maridhiano uliwasilishwa Mahakamani kuitaarifu Mahakama kumalizika kwa makubaliano hayo, ambapo Mhe. Kabururu alimtaka Mshtakiwa kukiri mashtaka yake.

Mnamo Septemba 18, 2025 baada ya kusomewa mashtaka na hoja za awali mshtakiwa alikiri kosa hilo na kutia saini makubaliano ya mkataba huo ambapo Mahakama ilimtia hatiani na kupewa adhabu ya kurejesha kiasi cha Tsh. 24,182,020/= kwa NHIF na kifungo cha nje cha miezi mitatu na fedha Tsh. 12,091010/= zimesharejeshwa NHIF na kiasi kilichosalia kitalipwa kwa awamu.

No comments:

Post a Comment